2014-04-24 08:41:49

Yohane Paulo II: utu na heshima ya binadamu na mshikamano kwa ajili ya maendeleo endelevu!


Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican inaendelea kukujuza mchango wa Mwenyeheri Yohane Paulo II katika kukuza na kudumisha Mafundisho Jamii ya Kanisa. Miaka sita baadaye, Papa Yohane Paulo II anatoa waraka mwingine wa kijamii ujulikanao kama Solicitudo Rei Socialis (Kuhusu Maswala ya Kijamii), mnamo tarehe 30 Desemba 1987. RealAudioMP3

Lengo la kwanza ni kuadhimisha miaka 20 ya waraka wa kijamii, Populorum Progressio yaani Maendeleo ya watu uliokuwa umeandikwa na Papa Paulo VI, tarehe 26 Machi 1967.

Kama ulivyokuwa waraka wa Papa Paulo VI, hati ya papa Yohane Paulo II ililenga pia kwenye swala la maendeleo ya watu. Hapa, papa anasema kwamba, hata kama ilikuwa imekwisha pita miaka 20 tangu Papa Paulo VI alipoangalia swala la maendeleo, lakini bado hali ya watu wengi sehemu mbalimbali za dunia walikuwa wanaendelea kujikatia tamaa na umaskini wao bila kuona cheche yoyote ya maendeleo. Lengo la Papa katika waraka huu ni kutaja kwa majina vikwazo vya maendeleo, kuonesha njia has za maendeleo, kutoa muelekezo juu ya maendeleo ya kweli ya watu na kutoa maelekezo ya jinsi ambavyo vigezo hivyo vya maendeleo vingeweza kufanyiwa kazi.

Papa Yohane Paulo II anaangalia hali ya uhisiano kati ya mataifa kwa kuangalia tofauti zilizopo kati ya upande wa kaskazini na upande wa kusini mwa dunia. Katika mantiki hii, Papa anaona kwamba kuna mapungufu na utofauti mkubwa kati ya upande wa kaskazini ambamo mataifa mengi ni tajiri, na upande wa kusini ambamo wanaishi watu wengi ambao ni maskini. Katika hili, papa anasema kwamba familia ya binadamu imeingia kwenye mgogoro wa kimahusiano kati ya matajiri wachache na maskini wengi, mgogoro ambao ulisababisha migawanyiko katika familia ya mwanadamu.

Mgawanyiko wa kwanza ulikuwa kati ya Umoja wa Kisovieti na mataifa ya Mkataba wa Warsaw na mgawanyiko wa pili ulikuwa ni kati ya USA na nchi za NATO. Kasi ya mashindano ya silaha kati ya hizi pande mbili ilizidi kuongeza hali ya hofu na na uhasama duniani kote, jambo ambalo lilikuwa likiwaudhi hata nchi washirika wa pande hizi mbili. Papa Yohane Paulo II alionesha masikitiko na mahangaiko yaliyotokana na mgawanyiko huo katika familia ya mwanadamu.

Mgawanyiko huu ulionekana pia kati ya nchi tajiri na nchi maskini zaidi duniani, ambao ulijulikana kama mgawanyiko kati ya kaskazini na kusini mwa dunia, au mgawanyiko kati ya mataifa tajiri na mataifa maskini. Ila jambo lilikuwa linasikitisha zaid ni kuona kwamba , hata umoja wa mataifa ulikuwa umekwisha jiwekea mbinu mkakati wa kuondoa umaskini miaka ishirini iliyo kuwa imepita, ila hakuna mafanikio yoyote yaliyoonekana, mbaya zaidi, sehemu nyingine za dunia umaskini ulikuwa umeongezeka maradufu hadi kufikia kipindi ambamo SRS inatolewa.

Baba mtakatifu anatamka wazi kwamba, nchi tajiri zaidi duniani ndizo zilizokuwa kikwazo cha maendeleo ya nchi maskini kutokana na sera walizokuwa wanatunga na vizingiti walivyokuwa wanaziwekea nchi maskini. Kiuchumi ni kipindi cha dunia kuingia kwenye soko huria.

Nchi maskini zinaambiwa kwamba ili kuondokana na umaskini wanapaswa kufungua mipaka yao na kuruhusu soko huria kufanya kazi, kw masharti kwamba serikali zijiondoe katika wajibu wake wa kuiziwezesha jamii zao na kuruhusu ubinafsishaji wa sekta zote ambazo zilikuwa mikononi mwa serikali. Sekta kama: elimu, afya, uchumi, maendeleo ya umma, usafirishaji na sekta zingine zikabinafsishwa kwa lengo la kuleta maendeleo kwa nchi maskini zaidi duniani, maendeleo ambayo hadi leo hayajaonekana.

Papa anafanya ziara nyingi za kichungaji kwa ajili ya kuongelea juu ya haki, amani na umoja kati ya mataifa na ndani ya jamii zenyewe.pamoja na kwamba papa aliandika waraka huu kuadhimisha miaka 20 ya Waraka kuhusu Maendeleo ya Watu, Waraka huu ulimpatia pia fursa ya kutoa maoni na mafundisho yake kuhusu hali ya dunia ilivyokuwa hasa kwa kuzingatia hali za watu maskini zaidi duniani. Katika kuadhimisha miaka 20 ya Waraka huu, Papa Yohane Paulo II anaendelea kutilia mkazo kuhusu maendeleo ya kweli, ambayo si yale yanayotokana na ulimbikizaji wa mali, bali ni yale yanayompelekea mtu kukua kiroho na kimwili, kiakili na kimaadili.

Pengo kubwa lililokuwepo kati ya nchi maskini na zile tajiri lilimkera sana Papa Yohane II, na anasema kwamba, ndani ya dunia yetu moja kuna dunia nne na hali hii inatishia umoja wa watu na wa mataifa. Mbaya zaidi kwa papa ni masuala ya kitamaduni kama vile ujinga, ugumu wa kupata elimu ya juu, na mtu kukosa uwezo wa kushiriki katika kuendeleza taifa lake, unyonyaji na ubaguzi. Vile vile, nchi au mataifa kunyimwa haki ya kupanga mbinu na mikakati ya kujiendeleza kiuchumi vinaharibu uhuru wa nchi na vinaingilia taratibu zake na kuathiri uhuru wa nchi.

Tema inayotawala katika waraka huu ni ushirikiano kati ya familia ya watu kwa ajili ya maendeleo endelevu. Na ushirikiano kati ya watu kama alivyoelewa na kufundisha papa Yohane Paulo II si ule unaotokana na huruma kwa sababu ya dhiki za watu wengine bali ni mshikamano ni ile hali ya kudumu katika kutenda wema kwa manufaa ya kila mtu na manufaa ya watu wote, kwani kila mtu anapaswa kuwajibika kwa ajili ya wengine. Hivyo mshikamano si huruma inayotokana na kuguswa na hali ya mahangaiko ya watu, ni hali ya maisha ambayo inapaswa kuwa ni kiini cha mahusiano kati ya mtu na mtu na kati ya mataifa.

Mshikamano kadiri ya mafundisho ya Papa Yohane Paulo II unapaswa kutekelezwa ndani ya kila jamii na ndani ya jamii ya kimataifa. mshikamano unamhitaji na kumlazimu kila mtu katika jamii kumtambua kila mmoja kama mtu na si tu kama chombo au bidhaa . mshikamano unapinga aina yoyote ya, uonevu, unyonyaji na unyanyasaji na maangamizo ya watu wengine.

Zaidi ya hayo, katika ngazi ya jamii , mshikamano unalichangamotisha Kanisa na watu wote kuwa upande wa maskini na wote wanaokataliwa katika jamii na kuwasaidia katika kukidhi mahitaji yao msingi na haki zao kwa kuzingatia mafao ya wengi. Aliye na uwezo zaidi anapaswa kuwashirikisha wengine utajiri wake. Maskini, wakati wakidai haki zao halali, lazima pia watoe mchango wao katika kukuza maadili na manufaa ya wote na si tu kuwa wanifaikaji wa mali ya umma.

Mshikamano ni muhimu zaidi katika ngazi ya kimataifa . Kutegemeana kimataifa lazima kusimikwe katika hali ya kutambua kwamba matunda yote ya kazi ya uumbaji wa Mungu ni kwa ajili ya matunizi ya binadamu wote bila ubaguzi na kwamba upatikanaji wa mali asili ni kwa ajili ya faida ya wote. Mshikamano unapingana na aina yoyote ya ubepari unaofanywa na mataifa tajiri dhidi ya mataifa maskini, na unapinganga na utumiahi wa nguvu. Mfumo wa ushirkiano wa kimataifa unapaswa kusimikwa katika usawa wa watu wote na katika kuheshimu tofauti za mila na desturi zilizopo kati ya mataifa.

Mchango wa Papa Yohane Paulo II katika kuendeleza mafundisho jamii ya Kanisa unaweza kuelezewa katika maneno matatu: kuheshimu hadhi ya mwanadamu, kushirikiana na kusaidiana.

Imeandaliwa na Sr. Gisela Upendo Msuya.
Chuo Kikuu cha Kipapa cha Mtakatifu Toma wa Akwino.
Angelicum, Roma.








All the contents on this site are copyrighted ©.