Viongozi wa Kanisa wanalaani mauaji ya watu wasiokuwa na hatia!
Askofu mkuu Dieudonnè Nzapalainga wa Jimbo kuu la Bangui, Jamhuri ya Watu wa Afrika
ya Kati amelaani mauaji ya Padre Christ Forman Wilibona kutoka Jimbo la Bossangoa
aliyeuwawa kikatili katika maadhimisho ya Ijumaa kuu. Viongozi wa Kanisa wanawaalika
waamini na wananchi wote wenye mapenzi mema kuungana kwa pamoja ili kuombea amani
na utulivu nchini humo sanjari na kuendelea kujikita katika majadiliano yanayolenga
kudumisha mchakato wa haki, amani na upatanisho wa kitaifa.
Mauaji ya Padre
Christ Forman Wilibona yametokea siku chache tu baada ya kikundi cha Seleka kumteka
Askofu mkuu Nestor-Dèsirè Nongo Aziagbya wa Jimbo kuu la Bossangoa pamoja na Mapadre
watatu. Katika siku za hivi karibuni kumekuwepo na ongezeko la vitendo vya mauaji
ya kutisha Kaskazini Mashariki mwa Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati.
Viongozi
wa Kanisa wanawataka wananchi wa Afrika ya kati kuondokana na mauaji ya watu wasiokuwa
na hatia na kuanza kujikita katika mchakato wa upatanisho wa kitaifa. Wanatoa mwaliko
pia kwa Jumuiya ya Kimataifa kusaidia harakati za kurudisha tena utawala wa sheria
pamoja na kuwapokonya wana mgambo silaha, kwani wamekuwa ni chanzo cha mauaji ya watu
wasiokuwa na hatia.