Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika
mahojiano maalum na Radio Vatican anasema, maisha ya utakatifu ni jambo linalowezekana
na wala si kwa ajili ya watu walioshi kanne nyingi zilizopita.
Mwenyeheri
Yohane Paulo II na Yohane XXIII ni mifano hai kwamba, utakatifu unawezekana hata kwa
watu wa nyakati hizi, jambo la msingi ni kumfungulia Kristo moyo wako, ili aweze kutawala
na kuyaongoza maisha yako. Watakatifu ni kielelezo makini cha maisha adili na manyofu
mbele ya Mwenyezi Mungu.
Askofu Ngalalekumtwa anasema, alibahatika kumfahamu
Papa Yohane Paulo II kunako Mwaka 1974, alipokuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Krakovia,
Poland. Alipata bahati ya kufa hija ya maisha ya kiroho wakati wa Maadhimisho ya Mwaka
Mtakatifu kunako Mwaka 1975 na wakabahatika kwenda Krakovia, Poland. Walipokuwa huko
kama mahujaji, Papa Yohane Paulo II alifika kuwasalimia mahali walipokuwa wanapata
malazi.
Papa Yohane Paulo II alimteuwa kuwa Askofu na hatimaye kumwekwa wakfu
kuwa Askofu hapo tarehe 6 Januari 1989 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini
Vatican. Wakati wa hija ya kichungaji ya Baba Mtakatifu Yohane Paulo II nchini Tanzania,
kunako mwaka 1990, Askofu Ngalalekumtwa ambaye alikuwa ni Mwenyekiti wa Idara ya Liturujia
ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, alibahatika kuwa karibu na Baba Mtakatifu
Yohane Paulo II.
Alimsaidia kwa maandalizi ya Ibada kwa Lugha ya Kiswahili
na kwamba, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania lilikuwa ni kundi la mwisho kwa Mabaraza
ya Maaskofu kukutana na kuzungumza na Papa Yohane Paulo II wakati wa hija za kitume
zinazofanywa na Maaskofu Katoliki mjini Vatican walau kila baada ya miaka mitano.
Miaka tisa baadaye, Maaskofu wanakusanyika tena mjini Vatican kumwimbia Mwenyezi Mungu
utenzi wa shukrani kwa zawadi ya utakatifu wa maisha, aliyomkirimia Mwenyeheri Yohane
Paulo II ambaye walimwacha akiwa amezidiwa Hospitalini Gemelli, sasa ni Mtakatifu
mbinguni, matendo makuu ya Mungu!
Askofu Ngalalekumtwa anasema, katika maisha
ya ujana wake alibhatika kumfahamu Mwenyeheri Yohane XXIII na pia aliweza kushuhudia
shamra shamra za maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Watakatifu hawa wawili
ni kielelezo na changamoto kwa kila mwamini kwamba, utakatifu ni jambo linalowezekana,
jaribu nawe utaona siri ya mafanikio! Kila mwamini ajitahidi kuachana na uzembe katika
maisha yake kwa kujikita katika mchakato wa kutangaza Injili ya Kristo kwa uaminifu
mkubwa na kwa njia ya ushuhuda wa maisha adili na matakatifu.