2014-04-24 11:31:47

Onesheni furaha yenu kwa Kristo Mfufuka!


Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake kwenye Ibada ya Misa Takatifu, Alhamisi tarehe 24 Aprili 2014 kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha, kilichoko mjini Vatican amewataka waamini kushuhudia furaha inayobubujika kutoka kwa Kristo Mfufuka, ambaye anaendelea kutembea na watu wake katika hija ya maisha yao hapa duniani.

Baba Mtakatifu anasema, Yesu alipowatokea mitume wake, walishikwa na butwaa na wasi wasi wakadhani kwamba, walikuwa wanaona mzimu, badala ya kufurahi na kushangilia ufufuko wa Yesu.

Baba Mtakatifu anawataka Wakristo wote kuachana na woga usiokuwa na mashiko, bali watoke kifua mbele kushangilia ufufuko wa Yesu Kristo mkombozi wa dunia. Wajitahidi kumkaribia Yesu katika maisha yao ili aweze kuwakirimia furaha ya kweli, ili waanze kutembea katika mwanga wa Kristo Mfufuka. Baba Mtakatifu anawataka waamini kuachana na maisha ya Popo anayetawala nyakati za usiku, lakini mchana anajifungia wala hawezi kuonekana kwa urahisi.

Kwa njia ya Ufufuko wa Yesu, waamini wamekirimiwa furaha na maisha ya uzima wa milele, changamoto ya kumfuasa Kristo katika njia ya Heri za Mlimani kwa kushikamana naye! Yesu amefufuka kweli kweli na kamwe hawezi kuwaacha wafuasi wake watembee katika giza, hivyo maisha ya Mkristo ni majadiliano endelevu na Kristo, ili aweze kuwasaidia katika hija ya maisha yao hapa duniani.

Waamini wanaoshindwa kuonesha furaha yao kwa Kristo Mfufuka, anasema Baba Mtakatifu Francisko ni watu waliobaki Ijumaa kuu, watu wasiokuwa na matumaini katika ufufuko wa Kristo. Anawaombea wote hawa ili Mwenyezi Mungu aweze kufungua akili na mioyo yao wapate kuyafahamu Maandiko Matakatifu, ili hatimaye, waweze kukutana na Yesu Kristo Mfufuka!







All the contents on this site are copyrighted ©.