2014-04-24 08:51:44

Mwaka wa waamini walei na changamoto zake!


Baraza la Maaskofu Katoliki Ufilippini linaadhimisha Mwaka 2014 kwa ajili ya wa Waamini Walei kwa kuwataka kuonesha ushupavu wa maisha ya kiimani, kwa kujikita katika ari na utume wa kimissionari sanjari na kukoleza majadiliano ya kidini na kiekumene miongoni mwa wananchi wa Ufilippini. RealAudioMP3

Hii ni changamoto ya kuwaonjesha watu wote upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake. Maadhimisho ya Mwaka huu yanaongozwa na kauli mbiu “ chagua kuwa jasiri”.

Waamini wanahamasishwa kuonesha ujasiri wa kiimani kwa kuwashirikisha wale ambao kutokana na sababu mbali mbali katika safari ya imani yao wamejikuta wakilega lega katika maisha ya Kikristo, ili waweze kupata ari na mwamko mpya, tayari kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa. Kampeni ya maadhimisho ya Mwaka wa Waamini Walei inavihamasisha vyama vyote vya kitume vinavyoongozwa na kusimamiwa na waamini walei kujitosa kimasomaso kuwasaidia waamini wanaokabiliana na utepetepe wa imani. Kampeni hii imezinduliwa hivi karibuni na Baraza la Maaskofu Katoliki Ufilippini.

Maaskofu wanasema, Familia yote ya Mungu nchini Ufilippini inaalikwa kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa, kwa kutangaza na kushuhudia imani na ukweli unaofumbatwa katika maneno, lakini zaidi kwa njia ya matendo. Waamini Walei wanahamasishwa kuwa jasiri katika imani, kwa kuwashirikisha waamini ambao wanalega lega ili waweze kuanza tena upya pamoja na kuzisaidia familia kutekeleza dhamana na wajibu wake katika Kanisa na Jamii kwa ujumla.

Waamini wanachangamotishwa kuwaendea wanandoa walioachana na kuangalia jinsi ambavyo wanaweza kuwapatanisha tayari kufungua ukurasa mpya wa maisha yao ya Kikristo. Maaskofu wanatambua kwamba, vijana ni jeuri ya Kanisa na Taifa, kumbe, wanapaswa kusaidiwa kikamilifu katika majiundo na malezi yao, ili waweze kuwa kweli ni vyombo vya Uinjilishaji Mpya miongoni mwa vijana wa kizazi kipya.

Maskini, watu wasiokuwa na fursa za ajira pamoja na wale wasiokuwa na makazi maalum wanaongezeka maradufu nchini Ufilippini kutokana na maafa asilia pamoja na athari za myumbo wa uchumi kimataifa, Kanisa linaalikwa kuwaangalia na kuwasaidia watu kama hawa ili waweze kuwa na matumaini kwa Kristo na Kanisa lake. Wakulima, wafugaji na wavuvi; walimu na wanataaluma katika nyanja mbali mbali za maisha pamoja na wananchi asilia ni makundi ambayo yanapaswa kuoneshwa upendeleo wa pekee katika hamasa ya kushiriki Mwaka wa Waamini Walei nchini Ufilippini.

Juhudi zote hizi zinafanyika katika ngazi ya Kitaifa, Kijimbo, Kiparokia pamoja na kuendeleza mikakati iliyobainishwa na vyama vya kitume katika ngazi mbali mbali mintarafu maagizo ya Baraza la Maaskofu Katoliki Ufilippini. Waamini walei wanahamaishwa kushirikisha tafakari, majadiliano na maamuzi mbali mbali kwa njia ya mitandao ya Jamii kwani hii pia ni njia mojawapo ya Uinjilishaji Mpya.

Baraza la Maaskofu Katoliki Ufilippini, linaendesha pia kozi maalum kwa njia ya mtandao na kuna idadi kubwa ya watu ambao wanashiriki. Katekesi ya kina inaendelea pia kutolewa kwa njia ya mtandao, lakini jambo la msingi ambalo waamini wanaendelea kuhamasishwa ni kutambua umuhimu wa kutolea ushuhuda wa imani katika matendo. Waamini wanapaswa kuwajibika na kushiriki kikamilifu katika maisha ya hadhara. Wasimame kidete kupinga rushwa, ubadhirifu wa mali ya umma na ufisadi; wawe thabiti katika kulinda na kutetea zawadi ya maisha, maadili na utu wema.

Imani katika matendo, ndiyo changamoto kubwa kwa Waamini walei nchini Ufilippini. Ukweli, uwazi, maadili na weledi ni kanuni zinazopaswa kuongoza matumizi ya fedha ya umma. Ni matumaini ya Baraza la Maaskofu Katoliki Ufilippini kwamba, Maadhimisho ya Mwaka wa Waamini walei, utazaa matunda ya toba, wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha miongoni mwa waamini nchini Ufilippini.








All the contents on this site are copyrighted ©.