2014-04-23 09:19:32

Utakatifu wa maisha!


Utakatifu ni hija ya maisha inayotekelezwa hatua kwa hatua kama walivyofanya Wenyeheri Yohane XXIII na Yohane Paulo II watakaotangazwa kuwa watakatifu, Jumapili ijayo kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Huu ndio utakatifu ambao watu wanaendelea kuushuhudia katika maisha na utume wa Wenyeheri hawa.

Padre Federico Lombardi, msemaji mkuu wa Vatican akiwa ameambatana na wahusika wakuu katika mchakato wa kuwatangaza Wenyeheri Yohane XXIII na Yohane Paulo II kuwa watakatifu: Padre Giovangiuseppe Califano pamoja na Monsinyo Slawomir Oder, Jumanne, tarehe 22 Aprili 2014, wamepembua maana ya utakatifu mintarafu maisha ya wenyeheri hawa wawili.

Yohane XXIII katika maisha yake kama Padre, Askofu na Khalifa wa Mtakatifu Petro alijiwekea nadhiri ya kuwa karibu na Yesu, kujificha katika Moyo wake Mtakatifu, Kusali Rozari na kumpatia nafasi ya pekee katika maisha yake. Haya ni mambo yaliyojionesha kwa namna ya pekee katika maisha na utume wake kama Mchungaji na Baba.

Ni kiongozi aliyeyasimika maisha yake katika furaha na ukarimu kiasi cha watu wengi kumwita kuwa ni Papa mwema! Alikazia umuhimu wa mshikamano katika maisha na utume wa Kanisa kwa kuitisha Sinodi ya Jimbo kuu la Roma na Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Ni kiongozi aliyeonesha upendo na uelewa katika shughuli za kichungaji; akawa kweli ni mtu wa msamaha na faraja kwa wote waliomkimbilia. Alikazia utii na amani ya kweli duniani.

Monsinyo Slawomir Oder anasema, utakatifu wa Mwenyeheri Yohane Paulo II ulianza kuonekana tangu alipokuwa bado Chuo Kikuu, kiasi kwamba, baadhi ya wanadarasa wake waliandika chumbani kwake, "Mtakatifu mtarajiwa", kutokana na na moyo na bidii ya sala, tafakari ya Neno la Mungu na maisha adili. Yote haya yalimwilishwa kwa njia ya matendo ya huruma.

Alikuwa na Ibada ya pekee kwa Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa, akawa na ujasiri wa kukabiliana na changamnoto za maisha kwa imani na matumaini pasi na kukata tamaa, kwani daima aliuona mkono wa Mungu ukiyaongoza maisha yake! Watu wengi walitambua kuwa kweli Yohane Paulo II alikuwa ni mtu wa Mungu aliyekuwa ni chemchemi ya maisha yake yote, kiasi cha kujikita katika Uinjilishaji Mpya, ili wote waweze kuwa ni watakatifu kwa kuonja huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao.







All the contents on this site are copyrighted ©.