2014-04-23 09:46:48

Tanzania imejaribiwa sana kiasi cha kuwekwa njia panda!


Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwaichi wa Jimbo kuu la Mwanza katika mahojiano maalum na Radio Vatican wakati huu wa Maadhimisho ya Siku kuu ya Pasaka 2014 anasema kwamba, Kristo Mfufuka amewapatanisha na kuwaweka watu huru, kiasi cha kurekebisha mahusiano yao katika ngazi mbali mbali. Katika hali ya mahusiano yaliyoponywa na kukombolewa, mwanadamu amekabidhiwa amani ambayo kimsingi ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, anayopaswa kuuishi na kuifanyia kazi. RealAudioMP3

Askofu mkuu Ruwaichi akizungumzia kuhusu hali ya wasi wasi, hofu na woga unaojionesha miongoni mwa Watanzania wakati huu wa mchakato wa Katiba pamoja na matukio kadhaa yaliyowaandama katika miaka ya hivi karibuni anasema, kamwe Mwenyezi Mungu hajawaacha watu wake. Mateso na mahangaiko ya watanzania yamesababishwa na watu kutompatia Mwenyezi Mungu kipaumbele cha kwanza katika maisha na mikakati yao.

Watanzania wengi ni waamini wa dini mbali mbali, hivyo wanachangamotishwa kuwa ni watu wanaojikita katika ukweli, unaowasukuma kutenda haki, kupendana na kuhangaikiana, kwa ajili ya mafao ya wengi, bila kuruhusu vitimbi vya ubinafsi wa mtu mmoja mmoja au makundi ya watu.

Askofu mkuu Ruwaichi anasema katika mchakato wa kuandika Katiba Mpya ya Tanzania, taifa la Tanzania limejaribiwa vibaya, kiasi hata cha kuwekwa njia panda. Yale yanayoendelea kujionesha kwenye mchakato wa kuandika Katiba Mpya ya Tanzania yanadhihirisha ukomavu au kutokomaa kwa watanzania katika masuala ya: imani, uzalendo, ukweli, haki, amani na umoja na mshikamano wa kweli pasi na unafiki!

Askofu mkuu Ruwaichi anasema kwamba, katika Kipindi hiki cha Maadhimisho ya Siku kuu ya Pasaka anapenda kuwaombea watanzania wote amani ya kweli na uthubutu wa watanzania wenyewe kuwa wakweli kwa kuona mbali badala ya kujitafuta wao wenyewe jambo ambalo ni hatari kubwa katika maisha!







All the contents on this site are copyrighted ©.