Mshikamano wa dhati kutoka kwa Papa Francisko kwa wafanyakazi wanaohofia hatima ya
maisha yao!
Baba Mtakatifu Francisko, mara baada ya Katekesi yake, Jumatano, tarehe 23 Aprili
2014 ameonesha masikitiko na mshikamano wake wa dhati kwa wafanyakazi wa kiwanda cha
kufua chuma, kilichoko Piombini, Kaskazini mwa Italia, waliomwomba kuwatembelea kabla
kiwanda hiki hakijafungwa.
Baba Mtakatifu anasema, nyuso za wafanyakazi hawa
zilionesha masikitiko makubwa na wasi wasi kuhusu hatima ya maisha ya familia zao.
Wafanyakazi hawa anasema Baba Mtakatifu wanachoomba ni haki ya kufanya kazi, ili waweze
kuishi kwa heshima, ili kuwatunza, kuwalisha na kuwaelimisha watoto wao. Baba Mtakatifu
amewahakikishia uwepo wake wa karibu kwa njia ya sala na kamwe wasikate tamaa, ili
kuamsha tena moyo wa matumaini yanayobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu, ambayo kamwe
hayawezi kudanganya.
Baba Mtakatifu anawaomba viongozi wanaohusika kujitahidi
kuhakikisha kwamba, wanatekeleza wajibu wao kwa kuzingatia kipaji cha ugunduzi na
ukarimu, ili kuwawashia tena matumaini wafanyakazi ambao wamekata tamaa kutokana na
madhara ya mtikisiko wa uchumi kimataifa, ambao umesababishwa na baadhi ya watu kutoguswa
na mahangaiko ya jirani zao.