2014-04-22 11:05:12

Vijana kutoka Jimbo kuu la Milano wafunika Roma!


Vijana 8,000 kutoka Jimbo kuu la Milano, Kaskazini mwa Italia, Jumatano, tarehe 23 Aprili 2014 wanatarajiwa kushiriki katika Katekesi ya Baba Mtakatifu Francisko na baadaye kuungama imani yao katika Makaburi ya miamba wa imani, ni watu waliyothubutu kuyamimina maisha yao kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake.

Hawa ni Mtakatifu Petro na Paulo. Lengo la hija hii ya maisha ya kiroho ni kuamsha ari na mwamko wa imani miongoni mwa vijana, ili waweze kuwa kweli ni mashahidi wa Kristo Mfufuka katika maisha yao!

Kardinali Angelo Comastri, Mhudumu mkuu wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa vijana hawa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, siku ya Jumanne, tarehe 22 Aprili 2014. Ibada hii imewashirikisha Mapadre mia mbili pamoja na umati mkubwa kwa walezi, wanaowasindikiza vijana hawa katika hija ya maisha yao ya kiroho.

Vijana wanafundwa namna ya kuheshimiana pamoja na kufanya maamuzi muhimu katika maisha yao, huku wakiendelea na malezi Parokiani mwao, ili kujenga na kuliimarisha Kanisa. Hija hii pia ni sehemu ya kumbu kumbu ya miaka mia moja tangu Jimbo Katoliki la Milano lilipoanzisha vituo vya kulelea vijana Parokiani.







All the contents on this site are copyrighted ©.