Ujumbe wa AMECEA kwa ajili ya Siku kuu ya Pasaka 2014
Tume ya haki na amani ya Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki
na Kati, AMECEA katika ujumbe wake wa Kipindi cha Pasaka inasema kwamba, Nchi za AMECEA
zimebarikiwa kuwa na utajiri mkubwa wa watu wema, wenye maisha na imani thabiti, lakini
wanaoishi kwa wasi wasi kutokana na kulega lega kwa misingi ya haki, amani na utulivu.
Sudan ya Kusini,
Malawi na Kenya ni kati ya nchi za AMECEA zinazohitaji sala maalum kwani zinakabiliana
na changamoto za uchaguzi ambazo mara nyingi zimekuwa ni chanzo cha uvunjifu wa misingi
ya haki, amani na utulivu.
Kunako Mwaka 2011, Sudan ya Kusini ilijipatia uhuru
wake, ikashangilia sana kama mwanzo wa matumaini mapya, amani, ustawi na maendeleo
ya wengi. Kwa takribani miaka arobaini, wanawanchi wa Sudan ya Kusini waliishi katikati
ya mtutu wa bunduki, kiasi kwamba, amani na utulivu ulikuwa ni msamihati mgeni kwao.
Miaka arobaini ya vita na mapambano ya wenyewe kwa wenyewe yalisababisha uharibifu
mkubwa wa miundo mbinu, huduma duni katika sekta ya elimu, afya na maendeleo ya watu
pamoja na umaskini mkubwa wa hali na kipato. Inasikitisha kuona kwamba, ndoto ya amani,
utulivu na maendeleo inatoweka taratibu na matokeo yake ni vita, umaskini, njaa na
maradhi kuanza kushika kasi.
Ni matumaini ya AMECEA kwamba, mchakato wa uchaguzi
mkuu nchini Malawi utakuwa huru, kweli na wazi, ili kudumisha misingi ya amani, utulivu
na maendeleo ya wengi. Kunako Mwaka 2009, Malawi ilifanya uchaguzi mkuu kwa amani
na utulivu na ikapongezwa na Jumuiya ya Kimataifa, ingawa kulikuwepo na kasoro ambazo
zilitaka kuzima mchakato mzima wa demokrasia ya kweli. Hakukuwepo na fursa sawa katika
kampeni, hali ambayo ilisababisha baadhi ya makundi kulalamikia hali hii, kiasi cha
kuzua kinzani na migongano ya kijamii. Ni matumaini ya AMECEA kwamba, uchaguzi mkuu
wa Mwaka 2014 utakuwa huru, kweli na wa haki.
Kenya ni nchi ambayo kwa miaka
ya hivi karibuni inaendelea kupambana na vitendo vya kigaidi vinavyotishia amani,
usalama na utulivu miongoni mwa wananchi wa Kenya. Wananchi wa Kenya wanakiu ya kuona
amani na utulivu vinatawala tena, ili kusaidia mchakato wa maendeleo endelevu. Ndiyo
maana AMECEA inawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kusali kwa
ajili ya kuombea amani na utulivu nchini Kenya.
Amani ni kati ya zawadi kubwa
ambayo Yesu Kristo Mfufuka aliwaachia wanafunzi wake. Amani ni tunda la haki na mapendo;
ni kikolezo cha maendeleo endelevu; mazingira ambayo yanamwezesha mwanadamu kuishi
utimilifu wa maisha. Kuna uhusiano mkubwa kati ya maisha na amani yanayobubujika kutoka
katika Fumbo la Pasaka yaani, mateso, kifo na ufufuko wa Kristo.
Huu ni mwaliko
wa kujenga na kudumisha amani na utulivu; umoja, upendo na mshikamano wa kidugu. Pasaka
ni kipindi cha kusherehekea amani na utulivu inayobubujika kutoka katika undani wa
maisha ya watu. Huu ni mwaliko wa kuelewa maana ya maisha mapya katika Kristo.
Na
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.