Salaam za Sikukuu ya Pasaka na matashi mema kutoka kwa Mwenyekiti wa Parokia ya Bikira
Maria Mama wa Huruma, Mbezi Beach, Jimbo kuu la Dar es Salaam tarehe 20/4/2014.
Wapendwa
Taifa la Mungu, Wana Familia ya BMMH Tumsifu Yesu Kristo ………. KRISTO AMEFUFUKA
KWELI KWELI………….
Salaam ya Kristo kwa wanafunzi wake baada ya Ufufuko ilikuwa
AMANI IWE KWENU Nami mtumishi wenu nisiyestahili kwa niaba ya Halmashauri ya Walei
ninawaalika tushiriki sote salaam hii ya Kristo Mfufuka nikiwatakia Amani yake itawale
katika mioyo yenu na katika familia zenu. HERI YA SIKUKUU YA PASAKA. ALELU………
Baada
ya Ijumaa kuu, leo kwa furaha tunasheherekea PASAKA, Hakika sisi sote ni watu wa
PASAKA na Haleluya ndio wimbo wetu, HERI YA SIKUKUU YA PASAKA - ALELU-----YAAA.
Taifa
la Mungu, Ufufuko wa BWYK uhuishe upya mioyo yetu katika kumtumikia “TAZAMA NAYAFANYA
YOTE KUWA MAPYA” nawaalika tuendelee kustawisha kanisa mahalia kwa kushiriki wote
kukamilisha ujenzi wa Jengo la Ofisi yetu ya Parokia. Na vigango kuendelea kukamilisha
vipau mbele vyao Aidha katika mwaka huu wa familia, Kanisa limeendelea kutoa kipaumbele
cha pekee kwa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia kwa kutambua kwamba, Familia
ni kitovu cha Uinjilishaji Mpya. Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba na tafakari
zake anawahimiza wanandoa kuhakikisha kwamba, wanajenga na kudumisha amani, upendo
na mshikamano wa dhati katika hija ya maisha yao ya kila siku.
Basi ninawaalika
kuitikia mwito huu wa kuzifanya familia zetu kuwa Makanisa madogo ya nyumbani, shule
ya amani, na darasa la furaha, haki , upendo na msamaha. Kwenu ninyi akina Mama,
ambao tumepewa dhamana ya kushiriki katika kazi ya uumbaji kwa kutunza zawadi ya maisha,
basi tuendelee kuwa waaminifu katika kutimiza wajibu huo mkubwa, Aidha Kristo ameamua
kututunza kwanza kwa kushuhudia zawadi ya ufufuko ikiwa pia ni ishara ya kuinuliwa
kwetu kutoka katika hali zote za ukandamizaji katika jamii. Tumshukuru na kufurahi,
Hakika Bwana ni mshindi. ALELU………
Taifa la Mungu wana Bikira Maria Mama wa
Huruma, kama mjuavyo nchi yetu ipo katika mchakato wa kuandika Katiba mpya, niwaalike
basi nasi kama sehemu ya watanzania tunaotumwa kutakatifunza malimwengu na kumleta
Kristo Mfufuka katika jamii zetu, ushiriki wetu katika kupata Katiba nzuri iliyosheheni
utu na uhuru wa kweli wa binadamu, tunu msingi za taifa, mgawanyo sawia wa rasilimali
za nchi, utawala bora na maadili ya viongozi. Kazi hii ni kubwa ; ni nyeti na tete,
kwani tunashuhudia malumbano makali yanayoendelea katika Bunge Maalum la Katiba,
malumbano haya yanatunyima usingizi na kupata hofu ikiwa kweli matumaini ya watanzania
yatafikiwa, tunajiuliza. Je, katiba mpya itafuta machozi ya watanzania wengi?
Basi, hii iwe sala yetu kuu kwa KRISTO Mfufuka, tusali, tuwasindikize wabunge
wa Bunge Maalum la Katiba kwa njia ya sala na majitoleo yetu ili Mwenyezi Mungu awaangazie
akili zao na kuimarisha utashi wao ili waweze kutekeleza dhamana hii nyeti kwa ajili
ya mafao ya watanzania wote hatimaye tupate katiba Mpya ambayo italinda na kudumisha
maendeleo ya sasa na kwa ajili ya vizazi vijavyo aidha, katiba itakayoendelea kujenga
na kuimarisha umoja na mshikamano wa kitaifa.
Taifa la Mungu, nimalizie kwa
kuwaalika kuendelea kuombea siku ya tarehe 27 Aprili 2014, ambapo Mapapa Wenyeheri
walioishi nyakati zetu watatangazwa kuwa watakatifu. Hawa ni Papa Yohane wa XXIII
na Papa Yohane Paulo wa II. Mababa hawa ni miamba wa Imani waliojitahidi kusoma alama
za nyakati kwa kutangaza maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican na kumwilisha
utume na maisha ya Kanisa katika ulimwengu mamboleo.
Ili kuwaenzi Mababa hawa,
kuna haja ya kujikita katika kutafuta kwanza mafao ya wengi, haki, amani na maendeleo;
kutetea zawadi ya uhai pamoja na kuwawezesha vijana katika kuwajengea mfumo wa maisha
adili na matakatifu kwa njia ya malezi bora ya familia. Niwashukuru wote kwa kufanikisha
Maadhimisho ya Juma kuu na hatimaye Siku kuu ya Pasaka KWAYA, MINISTRANT, WAHUDUMU,
WASOMA MASOMO, KAMATI TENDAJI K,P, WAPAMBAJI.NA WAAMINI WOTE. Niwatakie tena heri
ya PASAKA, NA MUNGU ATUKIRIMIE SOTE MEMA YAKE. ALELUYA Ni mimi Mwenyekiti wenu
– HW – Parokia Donesta Gisselle John Byarugaba.