2014-04-21 10:13:28

Mchango wa Papa Yohane XXIII katika mafundisho Jamii ya Kanisa


Papa Yohane wa XXIII alifundisha na kuishi kwa tabia ya uwazi na majadiliano, na alijitahidi kuwa bega kwa bega na mahangaiko ya kila mwanadamu. Katika waraka wake huu wa kwanza Mater et Magistra, Baba Mtakatifu anachambua hali ya utata katika mahusiano ya kijamii katika sekta ya jamii, alijaribu kutoa mikakati thabiti katika sekta ya kilimo, na anajadili kuhusu maswala ya mali binafsi na uhusiano wake katika jamii, na pia anajadili kuhusu swala la mishahara halali kwa wafanyakazi. RealAudioMP3

Huu ulikuwa ni waraka wa kwanza kuongelea kuhusu nchi changa ambazo zilikuwa zinaanza kupata maendeleo ya kiuchumi duniani. Walei katika waraka huu, walialikwa kutumia mbinu mpya katika kutazama maswala ya kijamii na kuzitumia katika kuendeleza Mafundisho Jamii ya Kanisa. Mbinu hizi zilikuwa ni: kwanza kabisa kuangalia jinsi mambo yalivyo, pili, kuyachambua kwa umakini ili kuyaelewa, na tatu, kutenda, yaani kutenda kadiri Kanisa linavyofundisha kuhusu maswala ya jamii. Mater et Magistra, yaani Kanisa ni Mama na Mwalimu, ni waraka wa kwanza wa kijamii wa papa Yohane wa XXIII, iliashiria nyakati mpya katika mafundisho ya jamii.

Maswala ya matatizo ya kijamii yanapewa kipaumbele cha kwanza kwenye mafundisho ya MM. Kwanza kabisa, baba mtakatifu anaona kwamba sekta mbalimbali za uchumi wa kisasa zilikuwa zinaendelea kwa viwango vya kutofautiana sana. Jambo ambalo alikuwa analiangalia kwa namna ya pekee ni swala la kilimo kwenye ulimwengu wa kisasa kama ulivyokuwa unajidhihirisha wakati ule. Si hilo tu, bali pia aliiona hali tete ya wafanyakazi waliokuwa wanaishi maeneo ya vijijini na mchango wao katika kuuendeleza uchumi.

Wazo jingine lilikuwa kwamba sekta zilizokuwa na uwezo mzuri kuichumi katika jamii ya nchi fulani, ilikuwa ni wajibu sekta tajiri ya taifa kuwasaidia wale wanaofanya kazi katika maeneo maskini ambayo watu wake hawakuwa na fursa ya kufurahia matunda ya maendeleo. Kisha, Papa anaendeleza mada hii katika kuongelea uhusiano kati ya mataifa tajiri na yale yaliyo maskini na mchango wa kanisa katika kwenye shida za jamii. Vile vile katika waraka wake huu anafuatilia kwa karibu mjadala kuhusu uhusiano wa ongezeko la idadi ya watu, maendeleo ya kiuchumi na hali ya ushirikiano wa kimataifa.
Mshahara halali na umoja wa wafanyakazi
Papa Yohane XXIII alionesha masikitiko makubwa yaliyosababishwa na kwamba alishuhudia kwa macho yake jinsi umati mkubwa wa wafanyakazi katika nchi mbalimbali walivyokuwa wanalipwa kiwango cha chini cha mishahara ambayo haikuwa inalingana kabisa na kazi walizokuwa wakizifanya. Na jambo hilo halikuwa likifanyika kwenye nchi moja tu bali kwenye nchi mbalimbali duniani. Papa alisisitizia tena umuhimu wa mshahara halali kwamba haupaswi kuamuliwa na nguvu za soko peke yake.

Papa alitoa mapendekezo au vigezo vinne vya kuzingatiwa: moja, katika kutoa mishahara inabidi kuangalia mchango wa watu katika kukuza uchumi; pili, hali ya kiuchumi ya makampuni ambao wafanyakazi wanafanya kazi; tatu kuangalia mahitaji ya kila jamii hasa kwa kuzingatia maswala ya ajira; na mwisho, kuzingatia manufaa ya watu wote, yaani manufaa ya mataifa mbalimbali ambayo yameungana kati yao ila yanatofautiana kwa asili na mahitaji.

Tabia ya soko huria ya kuhamishisa viwanda kwenye nchi au maeneo ambamo watu walikuwa wakilipwa kiasi kdogo tiu cha mshahara kwa masaa mengi ya kazi ilikuwa inaenda kinyume na mtizamo huu wa mshahara ulio halali. MM ilielezea swala la mahusiano ya kijamii kwamba lilikuwa la muhimu sana katika kipindi kile, kuongezeka kwa aina nyingi za mahusiano ya kijamii, yaani, ugumu unaojitokeza katika maisha ya watu ya kila siku kutokana na ukweli kwamba wanategemeana katika jamii na hivyo mahusiano hayaepukiki. Kutokana na hilo, alikuwa anatilia mkazo muundo wa vyama mbali mbali vya ushirika ili kuweza kukidhi haja za watu na mahusiano yao katika jamii.

Sehemu ya mwisho ya waraka huu kuhusu MM inaongelea juu ya kujenga upya mahusiano ya kijamii katika ukweli, haki na upendo. Hapa, baba mtakatifu ana waomba wanakanisa kujitokeza katika kusaidia mabadiliko ya maisha ya kijamii katika ulimwengu wa kisasa.

Imeandaliwa na
Sr. Gisela Upendo Msuya,
Chuo Kikuu cha Mtakatifu Thoma wa Akwino,
Angelicum, Roma.








All the contents on this site are copyrighted ©.