Askofu Munib Younan, Rais wa Shirikisho la Makanisa ya Kiluteri Nchi Takatifu na Yordan
katika ujumbe wake kwa Siku kuu ya Pasaka anawataka wananchi wa Israeli na Palestina
kujenga matumaini ya kuweza kuishi kwa pamoja katika misingi ya haki, amani na utulivu
pamoja na kuondokana na mashaka na wasi wasi, ambao umekuwa ni sehemu ya historia
ya maisha ya mwanadamu katika ulimwengu mamboleo.
Hii inaonesha kwamba, hali
ya kutoaminiana inaendelea kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Toma, aliyetia mashaka kuhusu
ufufuko wa Yesu. Wananchi walioko huko Mashariki ya Kati wanaendelea kuhoji ikiwa
kama mchakato wa kutafuta suluhu ya amani utapata muafaka, watu wameshikwa na wasi
wasi kuhusu vita na uvamizi; nyanyaso na dhuluma pamoja na uvunjifu wa haki msingi
za binadamu. Watu wana imani haba kama kiatu cha raba, kiasi hata cha kuhoji uwepo
wa Mungu katika maisha yao! Hii ni kutokana na kushamiri kwa vitendo ambavyo vinakwenda
kinyume cha mapenzi ya Mungu.
Katika ulimwengu mamboleo, bado kuna watu wanaotaka
kuhakiki kila jambo kama alivyofanya Mtakatifu Toma. Kwa watu wenye mashaka wanageuza
matumaini yao kwa viongozi wakuu wa Mataifa ili waweze kuwasaidia kuvuka vikwazo vya
kiuchumi na matumizi ya nguvu. Askofu Munib Younan anasema kwamba, Yesu alimfundisha
Mtakatifu Toma kuwa na imani na matumaini hata pale mambo yote yanapoonekana kukosa
mwelekeo.
Ufufuko wa Kristo ni tukio kubwa linaloshinda mashaka na wasi wasi;
nguvu ya watawala wa dunia hii; dhuluma, ukatili na misimamo mikali ya kiimani. Yesu
anaweza kuleta mwelekeo mpya wa historia ya maisha ya mwanadamu, ikiwa kama watamtumainia
bila mashaka!