Askofu mkuu mstaafu Boniface Lele kuzikwa Jimbo kuu la Mombasa 22 Aprili 2014
Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati, AMECEA linaungana
na Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya na kwa namna ya pekee na Familia ya Mungu Jimbo
kuu la Mombasa kuomboleza kifo cha Askofu mkuu mstaafu Boniface Lele, Jimbo kuu la
Mombasa kilichotokea hivi karibuni huko Mombasa kutokana na ugonjwa wa moyo.
Askofu mkuu
Tarcisio Zizaye, Mwenyekiti wa AMECEA katika ujumbe wake, anamshukuru Mwenyezi Mungu
kwa wema na ukarimu aliomtendea Marehemu Askofu mkuu mstaafu Lele katika maisha na
utume. AMECEA itamkumbuka sana kutokana na huduma makini aliyoifanya kwa Familia ya
Mungu nchini Kenya kama Padre, Askofu wa Jimbo Katoliki la Kitui na hatimaye, Askofu
mkuu wa Jimbo kuu la Mombasa.
Askofu Anthony Mueria wa Jimbo Katoliki Kitui,
Kenya anasema, wamepokea kwa masikitiko makubwa habari za kifo cha Askofu mkuu mstaafu
Boniface Lele, aliyewahi kuwa Askofu wa Jimbo la Kitui, kwa masikitiko makubwa, kwani
Askofu mkuu Lele ni kati ya Mapadre wa kwanza kabisa kutoka Jimbo Katoliki la Kitui.
Kwa Familia ya Mungu Jimboni humo, amekuwa kweli ni mfano bora wa kuigwa na Mapadre,
Watawa na Waamini katika ujumla wao.
Marehemu Askofu mkuu Boniface Lele alizaliwa
kunako tarehe 14 Aprili 1947, Kitui, Mashariki mwa Kenya. Baada ya masomo na majiundo
yake ya Kikasisi, akapewa Daraja Takatifu la Upadre tarehe 8 Desemba 1974. Kunako
tarehe 2 Februari 1996 akateuliwa na Mwenyeheri Yohane Paulo II kuwa ni Askofu wa
Jimbo Katoliki la Kitui.
Tarehe 1 Aprili 2005 akateuliwa kuwa Askofu mkuu
wa Jimbo kuu la Mombasa alikotumikia kwa moyo mkuu hadi tarehe 1 Novemba 2013 alipong’atuka
kutoka madarakani kutokana na sababu za afya. Taarifa kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki
Kenya zinaonesha kwamba, Askofu mkuu mstaafu Boniface Lele atazikwa tarehe 22 Aprili
2014 kwenye Kanisa kuu la Jimbo kuu la Mombasa. Ibada hii inatarajiwa kuanza majira
ya saa 4: 00 Asubuhi.
Maiti ya Askofu mkuu mstaafu Boniface Lele inatarajiwa
kutolewa kwenye Hospitali ya Pandya, jioni tarehe 21 Aprili 2014, ili kutoa nafasi
kwa Familia ya Mungu nchini Kenya kukesha na kuomboleza. Watu wengi wataendelea kumkumbuka
Marehemu Askofu mkuu mstaafu Lele kutokana na unyofu wake na bidii katika kuwahudumia
maskini na wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa Jamii. Hakutakuwa na uwekaji
wa mashada ya maua na badala yake, wale wanaotaka kununua mashada ya maua wanaweza
kutoa sadaka na mchango wao kusaidia maskini Jimbo kuu la Mombasa.