2014-04-19 07:15:40

Mmepata wapi ujasiri wa kwenda makaburini?


Taifa la Mungu Heri kwa Sikukuu ya Pasaka.

Mtu asiye na bahati au maskini akipata tunasema: Kipofu ameona mwezi. Maskini ni kama kipofu aliye gizani kwa vile haoni nuru yoyote ile katika maisha kwa vile hana kitu. Kadhalika mtoto anapozaliwa tunasema ameona mwanga. Anapokufa tunasema ameingia kwenye giza kaburini. Ukimwangalia mtu usoni, unatambua kwa hakika kwamba hajaumbwa kwa ajili ya kufa kwa vile anatafuta mwanga wa maisha. Daima mtu amekuwa akitafuta kwa namna nyingi sana kuijua siri iliyopo katika fumbo hili la kifo linalomtia uchungu na kumkatisha tamaa. Binadamu daima tunayatafakari na kuyaainisha maisha yake, lakini hata hivyo tunaona maisha hayo yanaishia kwenye giza la kifo.

Wataalamu mbalimbali wafilosofia wamejaribu sana kutafuta majibu ya kila aina ya kuanisha maisha kama vile, akina Sokratesi aliyetafiti juu ya mtima usiokufa lakini mwisho unabaki bado katika siri na fumbo hili bila kupata jibu kwa sababu hatima yake yote inakuwa ni kifo. Utasafiri katika barabara zote za maisha lakini mwisho unaingia kwenye barabara inayoongoza na kuishia kwenye giza la kifo. Wiki kuu tumeshuhudia matukio mbalimbali yaliyoongoza kwenye kifo cha Yesu mwenyewe aliyefika kutufungua macho juu ya kifo. Ama kweli “kama mti mbichi unaungua, Je, mti mkavu.” Hebu tuone jinsi Yesu mwenyewe anavyokipiga kifo rungu ya mwisho na kukimaliza kabisa, yaani kwa ufufuko wake.

Injili ya leo inaanza kwa kutuletea akina mama wawili waliokuwa wameshuhudia Yesu anapoteswa hadi kufa wanaenda kaburini alikozikwa. Wanaenda huko siku ya jumamosi (siku ya kwanza ya juma) karibu kuna bado usiku wa giza, mapema sana asubuhi ya siku ya kwanza. Kungali bado giza la kifo, yaani giza la kuondokewa na mwalimu wao mkuu waliyeishi naye. Ni giza toka Ijumaa kuu hadi siku hiyo ya kwanza ya juma. Kinaganaga hiki cha kueleza wakati huu, ina maana sana. Yaani kuna giza na kuna siku mpya. “Hata sabato ilipokwisha, ikipambazuka siku ya kwanza ya juma, Mariamu Magdalena, na Mariamu yule wa pili, walikwenda kulitazama kaburi.” Hasa maneno haya siku ya kwanza ya juma, hutupelekea kwenye neno la kitabu cha mwanzo, juu ya siku ya kwanza ya uumbaji. “Hapo mwanzo Mungu aliziuma mbingu na nchi. Nayo nchi ilikuwa ukiwa, tena utupu, na giza lilikuwa juu ya uso wa vilindi vya maji…Mungu akatenga nuru na giza. Ikawa jioni ikawa asubuhi siku ya kwanza”.


Ni siku ya kwanza ya juma, siku mpya inayoanza na nuru mpya. Hapa kuna juma mpya inayoanza tena inayoanza na nuru mpya. Nuru hiyo haina budi iangaze kutoka juu, na kuangaza kila kaburi kwa sababu mmejaa giza nene la kifo kinachotutisha binadamu wote. Nuru hiyo inaangaza katika giza la kifo ambalo binadamu kwa muda mrefu amefanya utafiti sana juu ya kifo katika giza la usiku kufanikiwa kupata jibu la maisha yao, sasa mapema asubuhi kunaingia mwanga kamili unaoangaza na kutoa maana ya lengo la maisha ya binadamu.


“Wanakuja Mariamu Magdalena, na Mariamu yule wa pili, walikwenda kulitazama kaburi.” Katika Injili hii ya Mateo, wametajwa akina Mariamu hawa wawili tu, yaonekana anakosekana mwanamke mmoja kwa sababu siku ya kumzika Yesu pale makaburini kulikuwa na wamama wengi waliosindikiza msiba kwa mbali na wamama watatu wanatajwa kwa majina. “Palikuwa na wanawake wengi pale wakitazama kwa mbali, hao ndio waliomfuata Yesu toka Galilaya, na kumtumikia. Miongoni mwao alikuwamo Maria Magdalene, na Mariamu mama yao Yakobo na Yusufu, na mama yao wana wa Zebedayo.” (Mt 27:55-57).


Hapa sasa anakosekana Mama ya wana wa Zebedayo. Akina mama hawa wawili wanaenda kaburini nadhani kwa ajili ya kuliangalia tu yaani, hawakuwa na lengo la kwenda kupaka mafuta maiti ya Yesu kama tunavyosikia katika Injili ya Yohane, kwa sababu isingeleta maana yoyote ile kupaka mafuta maiti baada ya kupita siku tatu. Walikuwa na desturi kama ya waafrika baada ya kuzika, siku za mwanzoni ni kwenda kulitazama kaburi, na kwa wamama hawa wawili naona ilikuwa kwenda kuangalia pengine kwa bahati mbaya pengine mfu aliyezikwa alikuwa bado hajafa sawasawa, lakini baada ya siku tatu unaweza kuwa na uhakika kwamba “Amekufa basi” hakuna matumaini tena ya uhai. Hii ndiyo ilikuwa hoja ya msingi ya kwenda kaburini. Yaani ni kuhakikisha kuwa giza la mauti linaendelea kama kawaida yake.


“Na tazama kulikuwa na tetemeko kubwa la nchi;” Mateo anaelezea mang’amuzi ya akina mama hawa kule makaburini kwa namna tofauti kuliko wanavyoeleza Wainjili wengine. Mathalani katika Injili ya Yohane, tunamkuta Maria Magdalena anayefika kaburini, anaona jiwe limeondolewa kaburini haoni zaidi anaondoka na kwenda mbio kuwahahabarisha mitume.

Petro naye anaondoka na kwenda kaburini kuhakikisha kilichotokea anatanguzana na mwanafunzi mwingine bila kumtaja jina. Kumbe Mateo anawaonesha wamama hawa wawili na vituko vingine vya kutisha vinavyoibuka pale kaburini: Na tazama palikuwa natetemeko kubwa la nchi; kwa sababu malaika wa Bwana alishuka kutoka mbinguni, akaja akalivingirisha lile jiwe akalikalia. Na sura yake ilikuwa kama umeme, na mavazi yake meupe kama theluji.” (Mt. 27:45.51-53). Hapa tunaletewa picha ya kibiblia ambayo mwinjili anataka kutuletea ujumbe wa kiteolojia ambao ni muhimu katika maisha yetu. Analeta picha hiyo ya kibiblia ili kutueleza ni nini kilitokea siku ya Pasaka. “Palikuwa na tetemeko kubwa la nchi” ni kama vile kusingekuwa kumetokea kabla yake kitu kama hicho katika historia ya ulimwengu.


Nchi inayotetemeka inaleta picha ya kama vile mama anayezaa, yaani anayeleta kiumbe kipya duniani, ndivyo nchi inatetemeka kwani inazaa mwanga na kuuingiza duniani yaani ufufuko, mwanga mpya wa kuangalia kifo. Ameleta ulimwengu mpya.


Mateo alituletea mtetemeko mwingine uliotokea Ijumaa kuu pale alipokufa Yesu. “Na tazama, pazia la hekalu likapasuka vipande viwili toka juu hadi chini, nchi ikatetemeka, miamba ikapasuka. Makaburi yakafunuka, ikainuka miili mingi ya watakatifu waliolala. Nao wakiisha kutoka makaburini mwao, baada ya kufufuka kwake, wakauingia mji mtakatifu, wakawatokea wengi.” (Mt 27:51). Lugha hii ni ya kiteolojia. Hapa mwinjili anataka kuonesha kwamba umetimia unabii wa Ezekiel. Aliyesema kwa jina la Mungu kwamba makaburi yenu yatafunguka. Ndiyo maana ya mtetemeko. Watu walikuwa wanazungumza juu ya giza, kifo cha mtima, ulimwengu wa giza. Sasa Mtu katika historia yake ameingia katika nyumba ya baba katika ulimwengu wa Mungu. Mambo ya kuharibika ya kuoza, ya kufa yameachwa duniani. Yesu amekuja kuleta maisha mapya ya Baba na siyo kuendeleza tena maisha ya hapa duniani ya kibaolojia. Bali maisha ya kudumu milele. Yeye ndiye aliyeleta aina hiyo ya maisha.


Picha nyingine tunayopata hapa ni ya malaika ikisema: “Malaika wa Bwana alishuka kutoka mbinguni, akaja akalivingirisha lile jiwe akalikalia.” Malaika anawakilisha uwepo wa Mungu, hiyo tena ni lugha ya kitaalilimumgu. Mwinjili Mateo anamwelezea kwa namna tofauti kabisa na wanavyoeleza waenjili wengine. Anatumia lugha ya kibiblia ili kuonesha ipi ilikuwa nafasi ya Mungu katika tendo hili zima la ufufuko. Kwa njia ya Malaika, Mungu ameliondoa jiwe lililokuwa limefunika kaburi. Lile jiwe lililokuwa limewekwa na binadamu kama alama ya ushindi wa kifo au kuonesha kwamba mbele ya kifo binadamu tumepandisha mikono na tumekubali sheria.

Kwamba binadamu hatuwezi kufanya chochote mbele ya kifo kinachowachukua ndugu zetu wapenzi. Kifo kimekuwa na neno la mwisho. Ndiyo maana hata hawa wamama wanaenda kaburini kuhakikisha ushindi huu mkuu uliojipatia kifo hata kwa Yesu. Waliweka hata jiwe kwenye kaburi lake kuonesha kwamba mambo yameisha kabisa, hakuna tena matumaini. “Funika kikombe mwanaharamu apite.”

Kumbe anakuja malaika na kufunua hilo jiwe. Mungu amefunua jiwe kwa daima, hakuna mwingine anayeweza kuliondoa. Siku ya Pasaka jiwe hili limefunuliwa na Mungu. Kisha Malaika anakaa kishujaa juu ya jiwe hilo kuonesha ushindi. “Na sura yake ilikuwa kama umeme, na mavazi yake meupe kama theluji.” Hii pia ni lugha ya kibiblia kuonesha sifa pekee za Mungu. Umeme ni sifa ya kimungu, ni picha inayoonesha ukuu na ukubwa wa hali ya juu kabisa unayoweza kumpatia Mungu peke yake. Kadhalika theluji iliyo nyeupe ni alama ya mwanga.


Sasa kutokana na Mungu kuingilia kati kitendo hiki hebu sasa uwaone askari walonda wanavyohaha: “Na kwa kumwogopa, wale walinzi wakatetemeka, wakawa kama wafu.” (Mt 28:4). Ni Mateo peke yake anayezungumza juu ya walinzi. Walinzi hao wana maana ya pekee sana hapa kwani wanawawakilisha walinzi wengine wanayeulinda ushindi wa kifo yaani mauti. Hao wanalinda kusudi wale wanaotaka kulifunua watoroke, maana yake wanataka jiwe lile libaki limefunika tu kaburi. Ni walinzi wale wanaolilinda jiwe lile lisifunuliwe ili kaburi libaki limefunikwa tu. Kumbe jiwe lile limefunuliwa. Mapato yake wale wanaolinda na kushikilia bado historia ya kifo wanatetemeshwa. “Wale walinzi wakatetemeka, wakawa kama wafu.”


Malaika anawaambia wale wanawake: “Msiogope ninyi!” Ni sawa na kusema, ninyi mnaofahamu maana ya ufufuko msiogopa, hawa wanaoogopa na kukilinda kifo ndiyo wanaotakiwa waogope. “Kwa maana najua ya kuwa mnamtafuta Yesu aliyesulibiwa. Sifa au cheo hiki cha Yesu ni muhimu yaani cheo cha “Msulibiwa” kwa sababu katika kutoa maisha yake pale Kalvari aliweza kudhihirisha jinsi gani Mungu anampenda binadamu. Hiyo ndiyo maana ya maelezo ya sifa na cheo hiki “Yesu Msulibiwa.” Pale Kalvari hapakuwa muda wa kukata tamaa, muda wa uchungu katika historia ya binadamu, na sasa tusilogwe kuisahau hali hiyo eti kwa sababu Amefufuka. La hasha, hicho ni cheo chake cha daima “Yesu Msulibiwa”, kwani ndiye aliyetupenda kiasi cha kutoa maisha yake msalabani.

Huyo “Yesu Msulibiwa” Hayupo hapa; kwani amefufuka kama alivyosema! Yaani, amepita hapa, lakini hayuko hapa, sanasana alipitia hapa kusafisha kaburi hili kwani yeyote aliyepita hapa ameshamwakilisha kwenye ulimwengu wa Mungu. Msiogope!


Woga unakuwepo kwa sababu tupo katika mazingira ya kifo, na kuendelea kukilinda kifo na woga. Ndiyo maana walinzi hawa hawajiruhusu na kukubali kufikirishwa na umeme na kuangazwa na mwanga wa Mungu kwa njia ya malaika mwenye sura kama umeme, na mavazi yake meupe kama theluji. Kwa hiyo utawaona walinzi hawa wa kifo jinsi watakavyoendelea kuwa upande wa madhara yanayoletwa na kifo, utaona jinsi watakavyohamasisha na kutumia pesa kuwapiga watu rushwa, kusema uwongo na kudanganyifu mwingi, kwa sababu watakazana juu chini kuuficha ukweli. Mbaya zaidi itakuwa kwa wale ambao hawataki kufungua macho yao kuona ukweli wataendelea kushikilia mali ya ulimwengu kama vile ingekuwa kitu muhimu cha mwisho hapa duniani.


“Amefufufuka kama alivyosema” Ushindi dhidi ya kifo, unaonekana kwa wale waliowahi kulisikiliza neno lake Yesu alipoongea. Jibu la fumbo hilo la ufufuko, haliwezi kufa kutokana na kufikiri bali kutokana na ufunuo wa Mungu mwenyewe kwa njia ya Kristo.

“ Njoni mpatazame mahali alipolazwa.” Malaika anawaalika wale wamama waende wakaone kaburi.

Mwaliko huo ni kwetu sisi sote pia. Tunaalikwa kwenda kaburini kuliangalia kaburi. Kutokuogopa kifo. Yabidi kukikazia macho kifo siyo kukiogopa. Siyo kulitoa kaburi kwenye fikra zetu kwa sababu kwa vyovyote kifo kinatutisha na kutufanya tusiwe binadamu. Yabidi kuingia na kutoka kisha kuwapasha habari hiyo wengine kamba tumeona kaburi tupu. Hayo tunaweza kuyafanya kwa njia ya maneno ya Yesu mwenyewe aliyowaagiza malaika: “Nendeni upesi, mkawaambie wanafunzi wake, ‘Amefufuka katika wafu.’” Yaani ameingia katika maisha mapya ya Mungu.


“Tazama, awatangulia kwenda Galilaya:” Ni mwaliko kwa wanafunzi kwamba amefufuka. Anataja Galilea kwani pahala ambako kulianzia ujumbe huu wote, taarifa zote za mahubiri yake na mwanga huu wote ulioingia duniani. Yabidi kuanza kule na kueleza kwa wote toka kule, kueleza kwa wote mang’amuzi ya Pasaka. Pale Ujumbe huu wa wanafunzi utakapoisha hubiriwa, basi macho yatafunguka.


Kufunguka macho siyo ya kibaolojia, bali mtazamo wa kiroho wa ndani, ambao wanao wale tu walio na moyo safi. “Heri walio na moyo safi maana watamwona Mungu.” Ndiyo malaika anapowaagiza: Mtakapokuwa mnawahubiria wengine kwamba kaburi ni wazi, mtakumbuka katika mioyo na akili zenu maneno ya mwalimu na kujiaminisha kwake, mtakuwa na mtazamo huo na mtaweza kuona mambo zaidi ya kaburi na kuona mwisho wa binadamu anayefuata kile kilichompata Yesu yaani kuingia mbinguni pahala alipo Mungu.


Malaika anaongeza kusema: “Haya, nimekwisha waambia.” Hali halisi ya ulimwengu ni kwamba daima tunaishi katika maisha haya pamoja na watu wenye kumtafuta na Mungu na wengine hawana habari kabisa. Wengine wanatushabikia na wengine unawaletea maudhi tu wanapokuona. Hiyo ndiyo hali halisi. Hii ndiyo Galilea yetu. Ni ulimwengu ambao inabidi tuhubirie mang’amuzi tuliyonayo kwa kusikiliza neno linalotufanya tumwone mfufuka, yaani wanawake wanaondoka toka kaburini wanaenda kuwahubiria wanafunzi.


Kuna makundi aina mbili ya watu wanaoondoka toka pale kaburini tena wote wanaondoka kwa haraka. Kundi la kwanza ndiyo hawa wamama walioona kaburi wazi, na kuna kundi la walinzi yaani wale wanaoendelea kutetea ulimwengu wa kale. Wamama wanaenda kutanga habari ya Pasaka, lakini hawa wengine wanaenda kutetea uwongo na kupinga ufufuko. Kwa hoja kwamba, kwa njia ya uwongo na hila unaweza kuendelea kuishi hapa duniani.


Mapato yake unayaona kuwa wamama hawa wanapoondoka wanakutana na Yesu anayewasalimu “Salamu!” Wao lakini “Wakakaribia wakamshika miguu, wakamsujudia.” (Mt. 27:9) Wamama hawa wanakutana na Yesu pale wanapokuwa njiani kwenda kutangaza na kuhabarisha wengine mang’amuzi yao ya imani. Kisha unaona tena jambo la kustaajabia na kujifunza kuona kuwa wamama hawa wanamshika Yesu miguu. Kuna nini cha pekee hadi washike miguu ya Yesu.


Kwa wabantu miguu inatumika sana kwa kutembea na mara nyingi inakuwa michafu kutokana na vumbi. Kwa hiyo “desturi ya kushika miguu” kwa mbatu humaanisha kuomba radhi, kujinyenyekesha, kama wafanyavyo akina mama wa kabila fulani la kibantu, kugaagaa miguuni pa mtu kama alama ya kumheshimu na kumpenda sana. Lakini kwa nafasi yetu hapa leo, miguu ina maana zaidi ya kutembelea katika safari ya maisha yetu hapa duniani.

Akina mama hawa wanapoishika miguu ya Yesu wanakumbuka miguu ile iliyopigiliwa msalabani, lakini haikubaki pale msalabani. Ikafanya safari na kwenda nbele zaidi. Kwani kule ilikoelekea hiyo miguu, tutafika hata sisi. Tunaalikwa kutafakari pamoja, wapi yataenda kufikia maisha yetu. Yataishia kule ambako yamefika miguu ya yule aliyeyatolea maisha yake kwa ajili ya kuwapenda ndugu zake binadamu. “Maisha safari tuende hodari, yapita taabu, yadumu thawabu.”

HERI KWA SIKUKUU YA PASAKA
Padre Alcuin Nyirenda, OSB.
All the contents on this site are copyrighted ©.