2014-04-19 07:56:37

Mapadre 10 kutoka Roma wapata chakula na Papa Francisko


Alhamisi kuu, Mama Kanisa ameadhimisha siku ile iliyotangulia kuteswa kwake, Yesu alipoweka Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na Daraja Takatifu kwa ajili ya huduma kwa Familia ya Mungu. Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi kuu mchana alipata chakula pamoja na Mapadre kumi kutoka Jimbo kuu la Roma, katika makazi ya Askofu mkuu Angelo Becciu, Katibu mkuu mwambata wa Vatican.

Baba Mtakatifu pamoja na Mapadre wenzake waliweza kukaa kwa takribani saa moja na nusu wakila na kubadilishana mawazo katika maisha na utume wa Kipadre. Hili ni kundi la Mapadre lililokuwa limeshiriki katika Maadhimisho ya Ibada ya kubariki Mafuta Matakatifu, iliyoongozwa na Baba Mtakatifu Francisko kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Hii ni mara ya pili kwa Baba Mtakatifu Francisko kula pamoja na baadhi ya Mapadre wa Jimbo kuu la Roma tangu alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki. Kwa njia hii, Baba Mtakatifu anaendelea kulifahamu Jimbo kuu la Roma na changamoto zake, kwani Mapadre hawa kila mmoja ameshirikisha uzoefu na mang'amuzi yake katika maisha na utume wa Kipadre Jimbo kuu la Roma.

Baba Mtakatifu amewasikiliza wote kwa utulivu pamoja na kuwatia moyo wale ambao wanakabiliana na hali ngumu katika maisha na utume wao kama Mapadre.







All the contents on this site are copyrighted ©.