Padre Federico Lombardi, msemaji mkuu wa Vatican anasema, Ibada ya Njia ya Msalaba
kuzunguka magofu ya Colosseo, Ijumaa kuu inatarajiwa kuhudhuriwa na umati mkubwa wa
waamini na mahujaji kutoka ndani na nje ya Italia. Baba Mtakatifu Francisko mara baada
ya Njia ya Msalaba anatarajiwa kutoa Neno kwa ajili ya kufunga tafakari ya Njia ya
Msalaba kuzunguka magofu ya Colosseo.
Wakati wa Njia ya Msalaba, watu mbali
mbali watasaidiana kuubeba kadiri ya tafakari zilivyoandaliwa. Hawa ni watu wenye
umri tofauti na kutoka sehemu mbali mbali za dunia, hali inayoonesha Ukatoliki wa
Kanisa. Jambo la msingi ni mateso na mahangaiko makubwa wanayokabiliana nayo watu
katika medani mbali mbali za maisha.
Padre Lombardi anasema Ibada ya Njia ya
Msalaba inaweza kuchukua muda wa saa 1:15. Ibada ya Njia ya Msalaba kuzunguka magofu
ya Colosseo itarushwa katika nchi zaidi ya 50 zitakazokuwa zimejiunga kutoka Kituo
cha Televisheni cha Vatican, CTV. Katika kesha la Pasaka, Wakatekumeni 10 watabatizwa
na Baba Mtakatifu Francisko, kati yao 5 ni kutoka Italia, wengine ni kutoka Bielorussia,
Senegal, Lebanon, Ufaransa na Vietnam.
Baba Mtakatifu katika Ibada ya Misa
Takatifu, Pasaka ya Bwana, ataadhimisha Ibada ya Misa peke yake na baadaye kutoa salam
zake kwa mji wa Roma na Ulimwenguni, maarufu kama "Urbi et Orbi". Hakutakuwa na salam
katika lugha mbali mbali kama ambavyo wengi wamezoea. Maadhimisho ya Pasaka kwa Mwaka
2014 yanavionjo vya kiekumeni anasema Padre Federico Lombardi.