Kardinali Angelo Comastri mhudumu mkuu wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican,
Siku ya Jumatano, tarehe16 Aprili 2014 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa wafanyakazi
wa Vatican kama sehemu ya maandalizi ya Siku kuu ya Pasaka, kwa kufanya tafakari ya
kina kuhusu busu la usaliti lililofanywa na Yuda Iskarioti kwa Yesu. Je, ni mambo
yepi ambayo waamini wanapaswa kujifunza kutoka kwa Yesu aliyemchagua na kumkabidhi
kutunza mkoba kwa ajili mahitaji ya mitume wake!
Kardinali Comastri anasema
Yesu anataka kuwafundisha mitume wake kwamba, kila mwamini asipokuwa makini na mwaminifu
kwa Yesu na Kanisa lake, anaweza kuwa msaliti mkubwa kiasi cha kuwashangaza watu.
Hata katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, bado kuna hatari ya kukutana
na kivuli cha Yuda Iskarioti, changamoto kwa kila mwamini ni kuhakikisha kwamba, anakesha
na kusali, ili asije akatumbukia katika kivuli cha Yuda na hapo atakiona cha mtema
kuni!
Mwenyezi Mungu anawapenda na kuwahurumia hata watu kama Yuda Iskarioti,
jambo la msingi ni kutambua dhambi hii na hivyo kukimbilia huruma na upendo wa Mungu
usiokuwa na kifani. Kwa bahati mbaya, Yuda Iskarioti hakuwa na fadhila ya unyenyekevu
wala hakuthubutu kuomba tena huruma na msamaha kutoka kwa Kristo na matokeo yake akatenda
dhambi kubwa zaidi ya kujikatia tamaa na huruma ya Mungu.
Kardinali Angelo
Comastri anasema, Mwenyezi Mungu anamkirimia kila mwamini nafasi ya kutubu na kumwongokea,
kumbe, hakuna sababu ya kujikatia tamaa kwa huruma na upendo wa Mungu, kwani hakuna
dhambi ambayo haiwezi kusamehewa mbele ya Mungu. Waamini wajenge ndani mwao moyo wa
toba na ari ya kutaka kumwongokea Mungu ili kuanza tena ukurasa mpya wa maisha yao
ya kiroho na kiutu!