2014-04-16 07:57:37

Mshikamano wa upendo wenye mashiko!


Malengo ya Maendeleo ya Millenia yaliyokuwa yamebainishwa na Jumuiya ya Kimataifa ifikapo Mwaka 2015 yalipania pamoja na mambo mengine kuleta mabadiliko makubwa katika maisha ya watu kwa njia ya mshikamano. RealAudioMP3

Malengo haya yalipania kutokomeza baa la njaa na umaskini duniani; kutoa elimu ya msingi kwa wote; kupunguza vifo vya akina mama wajawazito na watoto wenye umri chini ya miaka mitano; kukuza usawa wa kijinsia; kuboresha mazingira sanjari na kupambana na ugonjwa wa Ukimwi na Malaria duniani.

Kanisa Katoliki kwa njia ya Mashirika yake ya Misaada Kimataifa na Kitaifa, limekuwa ni kati ya wadau wakuu wanaoshiriki katika mchakato unaopania kuwaletea watu mabadiliko ya kweli katika maisha yao ya kila siku, kwa kumkomboa mtu mzima: kiroho na kimwili. Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki Hispania, “Manos Unidas”. Ni kati ya Mashirika ya Kimataifa ambayo yamekuwa mstari wa mbele katika kuendesha kampeni ya maendeleo kwa ajili ya nchi maskini zaidi duniani.

Kampeni hii imekuwa ikitekelezwa kwa takribani miaka 55 iliyopita. Mwaka huu, “Manos Unidas” linapenda kuendeleza mshikamano wa upendo na udugu kama sehemu ya mchakato wa kumletea mwanadamu maendeleo endelevu kwa kuzingatia: ukweli, haki, upendo na uhuru. Hizi ni kanuni msingi katika mchakato wa mabadiliko na maendeleo ya kweli kati ya watu anasema Bwana Soledad Suarèz, Rais wa Mano Unidas wakati wa uzinduzi wa Kampeni kwa Mwaka 2014. Kiasi cha Euro Millioni 44. 2 zilikusanywa katika kipindi cha Mwaka 2013, ikiwa ni pungufu ya kiasi cha Euro millioni 4.

Hiki ni kielelezo cha athari za myumbo wa uchumi kimataifa. Mano Unidas kuanzia Mwaka 2000 hadi Mwaka 2014 imekuwa ikishiriki kikamilifu katika Kampeni ya utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Millenia yaliyopitishwa na Umoja wa Mataifa, ingawa hadi sasa bado kuna mambo mengi ambayo utekelezaji wake umeyumba kutokana na sababu mbali mbali. Kuna haja ya kuendelea kudumisha mshikamano wa upendo na udugu kati ya mataifa kama sehemu ya mchakato wa kukabiliana na matatizo pamoja na changamoto mbali mbali za maisha ya mwanadamu.

Kampeni hii inalenga pia kusitisha biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo unaodhalilisha utu na heshima ya binadamu, kwa kuwajengea watu uwezo wa kiuchumi ili kuondokana na kishawishi cha kutaka kupata fedha kwa njia ya mkato. Watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi, wanapewa kipaumbele cha pekee ili kuwasaidia watoto hawa kurudi na kuishi katika familia zao. Manos Unidas, imechangia kwa kiasi kikubwa maboresho katika sekta ya elimu, afya, kilimo na maendeleo ya wanawake.

Kardinali Antonio Maria Rouco Varela, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Madrid anasema, Kampeni ya Manos Unidas inakumbusha kwamba, kila mtu anahusika katika mchakato wa kuleta mabadiliko katika maisha ya watu kama wadau wakuu na wala si watazamaji. Manos Unidas inajikita kutekeleza dhamana ya kuleta mabadiliko katika maisha ya watu kwa kusukumwa na imani kwa Yesu na Kanisa lake.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.