Mchango wa Umoja wa Ulaya katika mapambano dhidi ya virusi vya Ebola
Umoja wa Ulaya umeamua kuongeza msaada wake katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ebola
kwa nchi zilizoko Afrika Magharibi kwa kutoa kiasi cha Euro millioni moja. Msaada
huu utatumika kwa ajili ya kutoa matibabu pamoja na kupima athari zilizosababishwa
na ugonjwa wa Ebola sanjari na kutoa vipimo vitakavyosaidia kuharakisha upimaji wa
virusi vya Ebola kwa wagonjwa watakaokuwa wameambukizwa.
Hayo yamebainishwa
na Kristalina Georgieva, Kamishina wa Umoja wa Ulaya anayeshughulikia ushirikiano
wa kimataifa, ambaye anakazia umuhimu wa kuharakisha mapambano dhidi ya virusi vya
Ebola, huko Guinea na nchi jirani ili kudhibiti maambukizi ya ugonjwa wa Ebola.
Takwimu
za hivi karibuni zinaonesha kwamba kuna watu 108 waliofariki dunia na wengine 168
wanadhaniwa kwamba, wameambukizwa virusi vya Ebola. Jumuiya ya Kimataifa kwa sasa
inaendesha kampeni dhidi ya virusi vya Ebola kwa kushirikiana na Wizara za Afya kutoka
katika nchi ambazo zimetikiswa na ugonjwa huu.