Biashara haramu ya binadamu inadhalilisha utu na heshima ya binadamu!
Wajumbe wa Baraza la Makanisa Duniani hivi karibuni walihabarishwa kuhusu ongezeko
la biashara haramu ya binadamu duniani hali ambayo ni ukiukwaji mkubwa wa haki msingi,
utu na heshima ya binadamu. Juhudi za kupambana na biashara haramu ya binadamu bado
hazijazaa matunda yanayokusudiwa na Jumuiya ya Kimataifa. Hii ni changamoto kwa viongozi
wa Makanisa kushirikiana kwa karibu zaidi na Serikali pamoja na vyama vya kiraia ili
kuzuia na kukomesha kabisa biashara hii ambalo kwa sasa ni janga la kimataifa.
Hayo
yamebainishwa na Joy Ngozi Ezeilo, mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa katika mapambano
dhidi ya biashara haramu ya binadamu wakati alipokuwa anazungumza na wajumbe wa Baraza
la Makanisa Ulimwenguni kuhusu masuala ya kimataifa na kwa namna ya pekee tatizo la
uhamiaji na utumwa mamboleo.
Biashara haramu ya binadamu ni vitendo vya jinai
vinavyojikita hasa katika biashara ya viungo vya binadamu, utalii wa ngono pamoja
na hitaji la nguvu kazi kwa bei nafuu ili kuzalisha faida kubwa zaidi. Wajumbe wa
mkutano huu, kwa kauli moja walisema kwamba, kuna haja kwa Viongozi wa Makanisa kusimama
kidete kushughulikia tatizo hili linalodhalilisha utu na heshima ya binadamu, kwa
kushirikiana na Serikali, Vyama vya kiraia pamoja na Umoja wa Mataifa.
Biashara
haramu ya binadamu nchini Nigeria imejionesha kwa namna ya pekee kwa wizi wa watoto
wadogo kutoka Hospitalini, Nyumba za kutunza watoto yatima pamoja na Kliniki, ambako
baadhi ya wanawake kutokana na umaskini na uelewa kidogo wamejikuta "wakitapeliwa
na kuingizwa mijini". Kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kusimamia haki msingi na
usalama wa wahamiaji. Takwimu zinaonesha kwamba, Mashirika ya kidini ni kati ya taasisi
ambazo zimekuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya biashara haramu ya binadamu.