2014-04-14 09:25:52

Yatakatifuzeni malimwengu kwa njia ya ushuhuda wa maisha adili


Francis wa Assisi kama ilivyokuwa kwa watakatifu mashuhuri ndani ya Kanisa, alikuwa ni kijana aliyependa kuvinjari na kufurahia maisha, hadi siku ile alipokutana na Yesu Msulubiwa, akamwambia asaidie kujenga nyumba yake. RealAudioMP3

Tangu siku hiyo, Mtakatifu Francisko wa Assisi akabadilika na kuwa mtu mpya, akajiweka mikononi mwa Kristo ili aweze kuwa ni chombo chake cha amani, upendo kwa maskini pamoja na utunzaji bora wa mazingira. Ni Mtakatifu aliyejitahidi kutoa nafasi kwa Roho Mtakatifu katika hija ya maisha yake, ili aweze kumwongoza na kumletea maisha mapya yanayoonesha utu mpya.

Kanisa ni Mama na Mwalimu anayewachangamotisha watoto wake kusimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu. Ni mwaliko kwa waamini walei kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ushuhuda wa maisha yao, yanayopania pamoja na mambo mengine kuibua na kujenga sera na mikakati ya uchumi na haki jamii; haki, maendeleo na mafao ya wengi.

Askofu mkuu Charles Chaput, wa Jimbo kuu la Philadelphia, Marekani anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuchunguza dhamiri zao ili kuangalia ikiwa kweli wamekuwa mstari wa mbele kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu, tangu pale mtoto anapotungwa mimba hadi mauti ya kawaida inapomfika kadiri ya mapenzi Mungu. Katika ulimwengu uliosheheni chuki, uhasama na kulipizana visasi, Je, Waamini wamejifunza kusamehe na kusahau? Wamejifunza kuwapenda, kuwaheshimu na kuwaombea adui na watesi wao?

Askofu mkuu Chaput anawauliza wazazi na walezi, wakati huu Mama Kanisa anapojiandaa kuadhimisha Sinodi Maalum ya Maaskofu kwa ajili ya Familia, ikiwa kama wamewajibika kikamilifu kama wazazi na walezi kadiri ya Mafundisho ya Kanisa na Kijamii kuhusiana na matumizi ya muda, maamuzi na matendo yao? Au wamewaachia watoto na vijana wao kuongozwa na ulimwengu, ambao umegeuka kuwa kweli ni tambaa bovu? Familia zinapaswa kuguswa na kuonja shida na mahangaiko ya jirani zao pamoja na kusimama kidete kulinda na kutetea mafao ya wengi.

Askofu mkuu Chaput anasema, wazazi, walezi na viongozi wa Kanisa wanapaswa kuwa kweli ni mfano wa kuigwa kwa maneno na matendo yao adili, kwani dunia ya leo hii inapenda kuona mifano hai na wala si kupepeta mdomo! Mifano hii ijioneshe kwa namna ya pekee katika maisha adili, manyofu na uchaji wa Mungu. Waamini wajifunze kuheshimu kazi ya uumbaji mintarafu kweli za Kiinjili.

Ndoa na Familia ni taasisi inayokabiliana na changamoto kubwa katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Watu wanataka kuwa na uhuru usiokuwa na mipaka kiasi hata cha kumng’oa Mungu katika maisha yao. Waamini wanapaswa kujiuliza swali la msingi, ikiwa kama wamekuwa kweli ni mfano bora wa kuigwa katika maisha ya ndoa na familia; wamesimama kidete kulinda na kutetea tunu bora za maisha ya ndoa kadiri ya mpango wa Mungu kwa mwanadamu.

Familia zitambue kwamba, ni shule ya haki, amani, huruma na mapendo. Je, tunu hizi msingi zinajionesha katika mahusiano yao na watu wengine sehemu za kazi, katika sera na mikakati ya kiuchumi; Je, kama Wakristo, kweli wamekuwa ni chombo cha haki, amani, upendo na mshikamano au ndo kwanza kabisa wamekuwa ni wapiga majungu na wavivu kazini.

Askofu mkuu Chaput anasema utakatifu wa maisha ni changamoto kwa watu wote na wala si kwa ajili ya kikundi Fulani cha Maaskofu, Mapadre au Watawa. Anauliza swali la msingi, ikiwa kama Familia za Kikristo zinajibidisha kuchuchumilia utakatifu wa maisha kwa njia ya: Tafakari ya kina ya Neno la Mungu linalomwilishwa katika matendo ya huruma na mapendo; ikiwa kama wamejenga na kuimarisha maisha yao katika Sala na Maisha ya Kisakramenti. Je, kama waamini wamewasaidia jirani zao kuchuchumilia pia utakatifu wa maisha?

Askofu mkuu Chaput, akimwangalia Mtakatifu Francisko wa Assisi katika ujana wake uliompeleka mchak mchaka! Anawauliza wazazi na walezi, ikiwa kama katika malezi na majiundo ya watoto na vijana wao, wanajitahidi kuwajengea moyo wa unyenyekevu, uchaji na ibada; upendo na mshikamano kwa ajili ya maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.

Ikumbukwe kwamba, kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, Wakristo wanaunda Familia ya Mungu inayowajibika. Kumbe, ndiyo maana, Kanisa linawachangamotisha watoto wake kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya baa la njaa, umaskini na ujinga; kujenga na kuimarisha mikakati ya kiuchumi, kwa ajili ya mafao na maendeleo ya wengi.

Waamini na watu wote wenye mapenzi mema wanapaswa kujitosa kimasomaso katika mapambano dhidi ya biashara haramu ya binadamu pamoja na kutetea haki msingi za wahamiaji na wakimbizi. Wakristo washirikiane na watu wenye mapenzi mema kupinga na kulaani madhulumu na nyanyaso za kidini, kwa kutetea uhuru wa kuabudu na dhamiri nyofu. Wakristo na watu wote wenye mapenzi mema, waguswe na mahangaiko ya watu sehemu mbali mbali za dunia, wawe tayari kuchangia kwa hali na mali kadiri ya nafasi zao ndani ya Jamii, huu ndio utandawazi wa kweli unaojengeka katika msingi wa udugu na mshikamano.

Askofu mkuu Chaput anawachangamnotisha waamini kuwa kweli ni vyombo vya Uinjilishaji wa Furaha na Mapendo. Kipindi cha Kwaresima, kiwasaidie waamini kwa namna ya pekee kabisa kukumbuka lile tukio la Yesu pale Mlimani Kalvari alipokuwa ametundikwa Msalabani, alipomwambia Bikira Maria “Mama tazama mwanao; na Mwana tazama mama yako”.

Kwaresima iwe ni fura ya kuonesha upendo wa dhati kwa Kristo na Kanisa lake na kuwapenda jirani; ni mwaliko wa kulihifadhi Kanisa mioyoni mwetu, kwa kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa. Yesu anawakumbusha Wafuasi wake kwamba, Yeye ni Njia, Ukweli na Uzima. Kwaresima kiwe ni kipindi cha kumfuasa Yesu kama walivyofanya Watakatifu kama vile Francisko wa Assisi ili kupata furaha ya kweli inayobubujika kutoka katika mwanga wa upendo wa Mungu.

Imehaririwa na
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.