Wakazi wa Roma mwaalikwa kushiriki Ibada ya Njia ya Msalaba- Koloseo Roma
Wakazi wa Jiji la Rome, nyote mnaalikwa siku ya Ijumaa Aprili 18, majira ya jioni
kujiunga katika Ibada ya Njia ya Msalaba, katika magofu ya Koloseo, itakayoongozwa
na Baba Mtakatifu Francisko. Katika Ibada hiyo tafakari zinaulenga mgogoro wa kiuchumi
na hali ya wahamiaji wanaopambana na maovu mbalimbali kimaisha hasa kwa vijana wengi.
Vijitabu vya Tafakari vinachapishwa Jumanne hii na Taasisi ya uchapishaji
ya Libreria Editrice Vaticana, kama ilivyoandikwa na Msgr. Giancarlo Bregantini ,
Askofu Mkuu wa Campobasso - Boiano , Kusini mwa Italia ambako kumekuwa na matukio
mengi ya kusikitisha ya wahamiaji wanaotafuta kuingia Italia. Katika tafakari hiyo
anasema, vituo 14 vya Mateso ya Yesu , pia ni sawa na mapigo ya dunia ya leo hasa
matukio ya wahamiaji na mateso ya watu, kama inavyojulikana kwa wachungaji wa
Jimbo la Kusini mwa Italia, ambako kumetokea mauaji yaliyosababishwa na sumu zinazo
toka katika taka, hali ya wafungwa wanaoishi katika msongamano mkubwa magerezani,
na wahamiaji.
Askofu Mkuu Giancarlo Bergantini anasema , ndani ya mti wa
msalaba wa Kristo, mna dhambi zote za watu , ikiwemo ukiukwaji wa haki zinazozalishwa
na mgogoro wa kiuchumi, na matokeo yake makubwa ya kijamii , kama vile uhaba wa kazi
, ukosefu wa ajira ,ughushi wa fedha , watu kujiua , rushwa na ufisadi. Yesu aliyabeba
yote hayo wakati akitembea katika njia ya mateso ya Kalvario, kwa ajili ya kutufundisha
kwamba, ndani ya maisha si kutoa jibu ovu kwa uovu lakini ni kujenga madaraja ya
mshikamano, na kuishinda hofu ya kutengwa , na kutafuta nguvu mpya za kisiasa kwa
ajili ya utafutaji majibu kwa matatizo ya kijamii kwa njia amani na maridhiano.
Askofu
Mkuu Bergantini anaendelea kuitafakari njia ya Msalaba katika eneo la Koloseo, hasa
akilenga katika mapigo ya dunia ya leo, na hasa hali ya wakimbizi na wahamiaji,
majeraha ya wanawake ambao ni waathirika wa unyanyasaji, viwewe vya watoto waliodhulumika
kijinsia, maumivu ya mama wale ambao wamepoteza watoto wao katika vita, katika dimbwi
la madawa ya kulevya au ulevi wa pombe kupindukia. Lakini anasema, kuanguka kwa
Yesu mara tatu katika njia ya Golgotha , kunatupatia mawazo ya uhakika yenye
matumaini katika kuyashinda majaribu. Hii ni sala kali kwa Mungu, aliyoitoa Yesu,
kwa ajili ya kuwaangazia wale wanaoutazama msalaba wake. Na hivyo sisi tunajifuza
kutoka kwa Kristo kukubali udhaifu, na kukataa kukatishwa tamaa au kushindwa na ovu
lolote. Badala yake, tuwe kama Simoni wa Krene , mtu ambaye alimsaidia Mwana wa Mungu
kuubeba msalaba, ambaye leo hii pia anatuambia kwamba, ni kukutana na kila mmoja
na kutoa msaada kujenga udugu, na kumgundua Mungu katika kila mwanadamu.