Ugonjwa wa kifua kikuu bado ni tishio kwa maisha ya watu wengi!
Shirika la Afya Duniani, WHO linasema, ugonjwa wa kifua kikuu bado ni hatari sana
duniani na unaendelea kuongezeka kwa kasi kubwa kwani kila mwaka kuna wagonjwa wapya
wa Kifua kikuu millioni tisa. Kifua kikuu ni ugonjwa ambao umeendelea kuwa sugu kwa
dawa nyingi. Inakadiriwa kwamba, kuna watoto millioni moja duniani ambao wameambukizwa
ugonjwa wa Kifua kikuu.
Jambo la kusikitisha
wanasema wataalam wa ugonjwa wa Kifua kikuu ni kwamba, watu wanaendelea kupuuzia uwepo
wa ugonjwa huu licha ya madhara yake makubwa katika afya za watu. Zaidi ya wagonjwa
450, 000 wana sumbuliwa na ugonjwa wa Kifua kikuu sugu, wadudu ambao wanaweza kutibiwa
kwa uhakika kwa asilimia 20% tu.
Utafiti wa ugonjwa wa Kifua Kikuu uliofanywa
kwenye Chuo Kikuu cha Havard, Marekani na kuchapishwa kwenye Jarida la “Lancet” unaonesha
kwamba, Bara la Asia lina idadi kubwa ya watoto wanaosumbuliwa na ugonjwa wa kifua
kikuu, Idadi yao inakadiriwa kufikia watoto 400, 000.
Bara la Afrika lina
watoto wenye ugonjwa wa Kifua kikuu zaidi ya 280, 000. Ugonjwa wa Kifua kikuu Barani
Ulaya unaendelea kupungua sana na kwamba, kwa sasa kuna mpango mkakati wa kufuta kabisa
ugonjwa wa Kifua kikuu Barani Ulaya, ifikapo mwaka 2050. Wataalam wa ugonjwa wa Kifua
kikuu wanasema, mapambano bado yanaendelea na kwa sasa wameandaa “Skadi Mpya 10” zitakazorushwa
hivi karibuni kama sehemu ya mchakato wa kupambana na ugonjwa wa Kifua kikuu ambao
bado unaendelea kuwa ni tishio.
Makampuni 50 yanaendelea kufanya utafiti kuhusu
uhakika wa Skadi hizi katika kutibu na kuponya ugonjwa wa Kifua kikuu. Ili kufanikisha
tafiti mbali mbali kuhusu ugonjwa wa Kifua kikuu bado kuna upungufu wa dolla millioni
1.5 kila mwaka.