Mama Kanisa amelianza Juma kuu kwa maandamano makubwa Jumapili ya Matawi pamoja na
kukumbuka Mateso ya Kristo Msalabani kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu kutoka katika
lindi la dhambi na mauti. Alhamisi kuu, Mama Kanisa anakumbuka siku ile iliyotangulia
kuteswa kwake, Yesu alipoweka Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na Daraja Takatifu,
Sakramenti zinazomwilishwa katika huduma ya mapendo na udugu. Hii ni siku ambayo Makleri
wanarudia tena ahadi zao za utii kwa Maaskofu mahalia pamoja na kubariki mafuta matakatifu.
Ijumaa kuu, Mama Kanisa anakumbuka kwa namna ya pekee kabisa, mateso na kifo
cha Kristo Msalabani. Hapa Msalaba unaonesha: hekima, huruma na upendo wa Mungu kwa
mwanadamu. Jumamosi kuu, Mama Kanisa anakaa katika kimya kikuu, ili kusubiria Ufufuko
wa Kristo kutoka katika wafu, tayari kumwimbia Alelluiya kuu kwa kumshangilia, mwaliko
kwa waamini kufa na kufufuka na Kristo kwa kuikata dhambi na nafasi zake.
Baba
Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa watumiaji wa mitandao ya kijamii anasema
kwamba, Juma kuu ni muda uliokubalika kwa waamini kumuungamia Mungu dhambi zao na
kuanza kutembea katika njia nyofu!