Baba Mtakatifu Francisko amemwandikia ujumbe wa matashi mema na kheri Rabbi mkuu wa
Jumuiya ya Wayahudi mjini Roma Bwana Riccardo di Segni kwa ajili ya maadhimisho ya
Siku kuu ya Pasaka ya Wayahudi, hapo tarehe 14 Aprili 2014, itakayodumu kwa kipindi
cha siku nane.
Jumuiya ya Wayahudi inasema, imepokea kwa furaha na mikono
miwili ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko na kwamba, wao pia wanajiandaa kwa ajili
ya kumtumia matashi mema katika kipindi cha Pasaka.
Baba Mtakatifu anaiombea
amani Jumuiya ya Wayahudi iliyoko mjini Roma, wakati huu wanaposherehekea ushindi
wa kukombolewa kutoka utumwamini na mkono wenye nguvu. Pasaka kiwe ni kipindi cha
kukuza na kumwilisha huruma, upatanisho na mshikamano wa udugu kwa wote wanaoendelea
kuteseka katika utumwa mamboleo.
Baba Mtakatifu anayaelekeza pia mawazo yake
mjini Yerusalemu, anakotarajia kutembelea mwezi ujao, anawaomba wamsindikize katika
hija hii ya kichungaji kwa njia ya sala zao na kwamba, anaendelea kuwakumbuka na anawatakia
baraka tele!