2014-04-12 08:47:06

Sudan ya Kusini inahitaji msamaha na upatanisho wa kweli!


Askofu Rudolph Deng wa Jimbo Katoliki Wau, Sudan ya Kusini anasema, ili nchi iweze kusonga mbele katika mchakato wa haki na amani, kwa kuzingatia mafao ya wengi na ustawi wa wananchi wote wa Sudan ya Kusini, kuna haja kwa pande zinazosigana kusameheana na kuanzisha mchakato wa upatanisho wa kitaifa. Watu wamechoka kusikia mlio wa mtutu wa bunduki, wanataka amani, usalama na maendeleo ya kweli yanayozingatia mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Anasema, inasikitisha kuona kwamba, Sudan ya Kusini ambayo ni kati ya Mataifa machanga kabisa duniani, iliyojipatia uhuru wake kwa taabu na mahangaiko makubwa kunako mwaka 2011, imejikuta ikitumbukizwa katika vita ya wenyewe kwa wenyewe, hapo Desemba 2013.

Askofu Deng anakubaliana kimsingi na wazo la kuanzisha Jukwaa la amani na upatanisho, litakalojikita katika majadiliano yanayolenga kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani na upatanisho wa kitaifa. Ili kuweza kufikia lengo hil, kuna haja kwa Serikali na wadau mbali mbali kuhakikisha kwamba, wanawaandaa watu watakaweza kutekeleza jukumu hili nyeti kwa ajili ya mafao ya wengi.

Askofu Deng anasema, Sudan ya Kusini inaweza kuiga mfano wa Afrika ya Kusini iliyounda tume ya haki, ukweli na upatanisho kama sehemu ya mchakato wa kuponya madhulumu ya liyojitokeza wakati wa utawala wa ubaguzi wa rangi Afrika ya Kusini, leo hii wanasherehekea Miaka ishirini ya utawala wa kidemokrasia. Ni matumaini ya Askofu Deng kwamba, Afrika ya Kusini itaweza kuwapatia msaada wa kutosha katika utekelezaji wa changamoto ya ukweli na upatanisho nchini Sudan ya Kusini.

Wananchi wa Sudan ya Kusini hawana budi kujikita katika mchakato wa majadiliano ya yanayosimikwa katika ukweli na uwazi, kwani kukosa na kukoseheana ni sehemu ya ubinadamu, lakini kusamehe na kusahau ni mwanzo wa maisha mapya!







All the contents on this site are copyrighted ©.