2014-04-12 06:57:57

Jumapili ya Matawi mjini Roma kuongozwa na Papa Francisko!


Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa, Jumapili ya Matawi, Mama Kanisa anapomsindikiza Yesu kwa shangwe kuingia mjini Yerusalemu, ili kukabiliana na mateso, kifo na ufufuko wake, anatarajiwa kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Hii pia ni Siku ya ishirini na tisa ya Vijana Kijimbo, inayoongozwa na kauli mbiu "Heri maskini wa roho maana ufalme wa mbinguni ni wao". Baba Mtakatifu atabariki matawi na baadaye maandamano ya vijana yataanza kuzunguka Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro na mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko ataongoza Ibada ya Misa Takatifu, mwanzo wa Juma kuu.

Hii ni siku ambamo Mama Kanisa pia anakumbuka miaka thelathini tangu Mwenyeheri Yohane Paulo II alipowakabidhi vijana Msalaba wa Mwaka wa Ukombozi, Msalaba ambao umetembezwa sehemu mbali mbali za dunia, kielelezo cha imani, matumaini, mapendo na changamoto kwa vijana wa kizazi kipya!.







All the contents on this site are copyrighted ©.