2014-04-12 15:02:03

Historia ni mwalimu wa maisha!


Tume ya Kipapa ya Sayansi za kihistoria, Mwaka huu inaadhimisha kumbu kumbu ya miaka sitini tangu ilipoanzishwa na Papa Pio wa kumi na mbili na wakati wote huu, imelihudumia Kanisa kwa weledi na tija, kiasi cha kuliwezesha Kanisa kuwahamasisha walimwengu kutafuta ukweli unaojikita katika undani wa moyo wa wanadamu!

Baba Mtakatifu Francisko, akizungumza na wajumbe wa tume hii, Jumamosi, tarehe 12 Aprili 2014 amewakumbusha kwamba, katika tafiti na mafundisho yao wanakutana na Kanisa linalosafiri katika nyakati na historia yake ya Uinjilishaji, matumaini na mapambano ya kila siku; haya ni maisha ambayo yanajikita kwa namna ya pekee katika huduma ambayo si haba. Lakini kwa upande mwingine, wanaona ukosefu wa uaminifu, hali ya kukata tamaa na uwepo wa dhambi.

Baba Mtakatifu anawaambia kwamba, tafiti zao zikiwa zimesheheni upendo kwa Mama Kanisa na ukweli, zinaweza kuwa ni msaada mkubwa katika kung'amua kile ambacho Roho Mtakatifu anapenda kuliambia Kanisa kwa sasa. Tume hii ni sehemu ya ushirikiano na taasisi mbali mbali duniani, inayowasindikiza wasomi katika tafiti zao, kama sehemu ya mchango wa Kanisa katika kukuza na kuendeleza majadiliano na ulimwengu mamboleo.

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika kujiandaa kikamilifu katika maadhimisho ya Karne moja, tangu vita kuu ya kwanza ya dunia ilipofumuka na hivyo kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali. Ni vyema, wakaangalia kwa umakini mkubwa mchango wa Vatican katika masuala ya kidiplomasia, msaada uliotolewa na Wakristo katika kuwasaidia na kuwahudumia wakimbizi, wahamiaji na majeruhi wa vita; watoto yatima, wajane.

Papa Benedikto wa kumi na tano akizungumzia kuhusu vita hii aliwahi kusema kwamba, ni janga lisilokuwa na mashiko! Hata leo hii bado Mama Kanisa anaendelea kuhimiza kwamba, kwa njia ya amani hakuna kinachoweza kutoweka, lakini kwa vita kila kitu kinapotea. Maneno haya ya kinabii yaisaidie Jumuiya ya Kimataifa kutambua kwamba, historia ni mwalimu wa maisha.







All the contents on this site are copyrighted ©.