2014-04-11 14:41:32

WHO, yatoa mwongozo mpya kwa maradhi ya ini (Hepatitis C)


Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani (WHO), limetoa mwongozo mpya kwa ajili ya matibabu ya maradhi ya ini yanayojulikana kwa jina la “hepatitis C”, maambukizi sugu yanayotajwa kuathiri kati ya watu 130- 150 milioni duniani.

Mwongozo mpya una lengo kusaidia nchi kuboresha matibabu na huduma kwa maradhi ya ini na hivyo kupunguza vifo vinavyotokana na kansa ya ini. Dk Stefan Wiktor ,Mkuu wa Mpango wa kukabiliana na Maradhi ya ini wa WHO, ameeleza katika ripoti yake.

Mwongozo huo uliochapishwa , unakwenda sanjari na upatikanaji wa dawa zinazofaa zaidi , kutibu Hepatitis C, pamoja na ahadi ya dawa mpya zaidi zitakazo tolewa katika miaka michache ijayo , kwa ajili ya kukabiliana na ugonjwa, unao sababisha vifo 350,000 hadi 500,000 kwa mwaka .

WHO sasa inafanya kazi ya kuingiza mwongozo huo, kama sehemu ya mipango matibabu ya kitaifa. Msaada wa WHO, ni pamoja na uwezeshaji wa matibabu mapya, na wazo la uwezekano wa tiba hiyo kupatikana kwa gharama nafuu kwa watu wote , kama vile uwepo wa vipimo bora kutahimini hali ya ugonjwa na aina ya dawa inayoitikia vyema kutibu hepatitis C.

Mpaka sasa tiba ya Hepatitis C ni ghali kwa wagonjwa wengi. Na hivyo, changamoto mpya sasa ni kuhakikisha kwamba kila mtu anaye hitaji madawa haya, anaweza kuyapata, anasema Dk Peter Beyer , Mshauri kwa ajili ya Madawa muhimu na vifaa, wa Idara ya Afya , WHO.

Mwongozo mpya , ulizinduliwa katika mkutano wa Kufungua mwaka 2014 wa Kongamano la Kimataifa, kwa ajili ya maradhi ya ini , lililofanyika London, ambalo lilikamilika kwa kutoa mapendekezo muhimu tisa . Mapendekezo hayo ni pamoja na mbinu ya kuongeza idadi ya watu kupimwa maambukizi ya hepatitis C , ushauri na jinsi ya kukabiliana na uharibifu wa ini kwa wale walioambukizwa na jinsi ya kuchagua na kutoa matibabu sahihi kwa muda mrefu kwa walioshikwa na hepatitis C.
Hepatitis C huenea kwa njia ya kuwasiliana na damu yenye vimelea, kwa kutumia pamoja sindano zenye vimelea, kuongezewa damu yenye vimelea, maambukizi kutoka kwa mama kwa mtoto mchanga wakati wa kujifungua, kwa njia ya kujamiiana, utumiaji wa sindano chafu kutoa damu kwa ajili ya vipimo, kushirikiana nyembe za kunyolea ndevu, miswaki, na mambo mengine yanayoweza kuingiza damu yenye vimelea hepatitis C kwa mtu mwingine.

WHO inasema, mtu hawezi kupata ambukizo la hepatitis C kwa kuishi au kuwa karibu , au kumgusa mtu mwenye ugonjwa huo, isipokuwa kwa njia zilizotajwa hapo juu. Aidha kwamba, kwa asilimia 30% chanzo cha maambukizi ya ugonjwa huu hakijulikani hasa hepatitis C sugu.

Dalili za kuwa na ugonjwa, watalaam wanasema, hakuna dalili za papo kwa papo wakati wa kwanza wa maambukizi. Takriban ya 80% ya wagonjwa wapya dalili hazionyeshi nje. Na asilimia 20% iliyobaki ya wagonjwa wapya walioambukizwa huwa na za uchovu wa mwili, maumivu ya tumbo, kichefuchefu, upungufu wa hamu ya chakula, au kuwa na dalili za homa ya manjano, ambayo sehemu nyeupe za mwili kama macho na viganja kuwa na rangi ya njano. Na Wakati huo huo, mkojo inaweza kuwa na rangi ya hudhurungi. Dalili hizi kwa kawaida hujitokeza baada ya kupita kipindi cha wiki 4-12 tangu kuambukizwa na HCV. Baadhi ya watu huwa na dalili za joto la mwili kupanda au homa na wengine hujisikia kama vile wana mafua.
Watalaam wanashauri watu kujenga tabia ya kupima afya mara kwa mara, ili kugundua kasoro mapema katika maungo ya mwili.







All the contents on this site are copyrighted ©.