Siku za Vijana Duniani zinapania kukuza na kudumisha ari na moyo wa kimissionari
Baba Mtakatifu Francisko ana matumaini makubwa katika maadhimisho ya Siku za Vijana
Duniani kama nyenzo msingi inayopania kuwasha na kukuza ari na moyo wa kimissionari
miongoni mwa vijana ndani ya Kanisa. Ni maneno ya Kardinali Stanislaw Rylko, Rais
wa Baraza la Kipapa la Walei, wakati wa ufunguzi wa mkutano wa kimataifa wa wakurugenzi
wa utume wa vijana, unaofanyika mjini Roma kuanzia tarehe 10 hadi tarehe 13 Aprili
2014. Mikutano hii ni sehemu ya maandalizi ya Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani
itakayoadhimishwa Jimbo kuu la Krakovia, Poland, kunako mwaka 2016.
Mkutano
huu unahudhuriwa na wajumbe 250 kutoka katika Mabaraza ya Maaskofu Katoliki 90 na
Jumuiya za Kitume 45 sanjari na Kamati ya Maandalizi ya Siku ya Vijana Duniani Rio
de Janeiro na Kamati kutoka Jimbo kuu la Krakovia. Kardinali Rylko anasema, katika
maadhimisho ya Siku ya Vijana Kijimbo, itakayofanyika Jumapili ya Matawi, kwenye Uwanja
wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Baba Mtakatifu Francisko atawakabidhi
rasmi vijana kutoka Poland Msalaba wa Siku ya Vijana Duniani, uliotembezwa nchini
Brazil kama sehemu ya maandalizi ya Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani yaliyokofanyika
nchini Brazil.
Tukio hili ni muhimu sana kwa mwaka huu, kwani Mama Kanisa anaadhimisha
kumbu kumbu ya Miaka thelathini, tangu Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili, kunako Mwaka
1984 wakati wa Siku kuu ya Pasaka sanjari na kufunga rasmi Mwaka wa Ukombozi, alipowakabishi
vijana Msalaba wa Mwaka wa Ukombozi. Ni Msalaba ambao umetembezwa sehemu mbali mbali
za dunia kwa kuwasindikiza vijana katika shida na mahangaiko yao bila kusahau furaha
na matumaini yao kwa Kristo na Kanisa lake.
Msalaba wa Mwaka wa Ukombozi, umekuwa
ni alama ya toba na wongofu wa ndani, chemchemi ya miito mitakatifu ndani ya Kanisa
na kwamba ni Msalaba ambao kweli umekuwa ni kikolezo cha imani na matumaini miongoni
mwa vijana wa kizazi kipya. Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani, kama alivyosema
Baba Mtakatifu Francisko nchini Brazil ni maadhimisho ya imani na udugu na kwamba,
hii ni zawadi kubwa kwa Mama Kanisa.
Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani
kwa Mwaka 2016 yatafanyika nchini Poland, miaka 25 tangu yalipofanyika kwa mara ya
kwanza nchini Poland kunako mwaka 1991 mara tu baada ya kuanguka kwa Ukuta wa Berlin.
Hapo dunia ikashuhudia nguvu na jeuri ya vijana waliomiminika kutoka sehemu mbali
mbali za dunia ili kuungana katika maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani, kwa pamoja
wakaimba, ule wimbo maarufu "AbbĂ , Padre", unaoendelea kuvuma sehemu mbali mbali za
dunia.
Tangu wakati huo anasema Kardinali Rylko, kumekuwepo na mabadiliko makubwa
sana ulimwenguni na ndani ya Kanisa. Kuna mabadiliko makubwa katika ulimwengu wa vijana
wanaoogelea katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia.
Kumbe, maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani ni kikolezo cha ari na mwamko wa kimissionari,
kwa kutafuta na kuibua mbinu mkakati kwa ajili ya utume wa Mama Kanisa kwa vijana.
Kwa
namna ya pekee, wakati huu, Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kukazia umuhimu wa
upendo na huruma ya Mungu; toba na wongofu wa ndani. Mama Kanisa anajiandaa kuadhimisha
tukio la kihistoria kwa kuwatangaza Wenyeheri Yohane XXIII na Yohane Paulo II kuwa
watakatifu hapo tarehe 27 Aprili 2014. Kanisa katika maadhimisho ya Siku ya Vijana
Duniani itakayofanyika nchini Poland kunako mwaka 2016, itamkumbuka Papa Yohane Paulo
II muasisi wa Siku za Vijana na Msimamizi wa maadhimisho ya Siku za Vijana Duniani.
Mwenyeheri Yohane Paulo II kwa vijana ataendelea kuwa ni Baba na Rafiki; Mlezi
na Msimamizi wa vijana mbinguni. Mkutano huu umefanya pia tathmini ya maadhimisho
ya Siku ya Vijana Duniani iliyofanyika Rio de Janeiro, Brazi, pamoja na kuangalia
matunda ya shughuli za kichungaji yaliyopatikana wakati wa maadhimisho ya Siku ya
Vijana Duniani nchini Brazil kwa njia ya ushuhuda na taarifa mbali mbali zilizowasilishwa
na wajumbe.