2014-04-11 08:58:08

Onesheni ujasiri kwa kujikita katika majadiliano ya amani na upatanisho wa kitaifa!


Baba Mtakatifu Francisko amemwandikia Rais Nicolàs Maduro Moros pamoja na viongozi wa vyama vya upinzani nchini Venezuela kuwashukuru kwa mwaliko walioutoa kwa Vatican kuweza kushiriki katika mchakato wa majadiliano ya amani na upatanisho wa kitaifa, ili kuponya madonda ya machafuko ya kisiasa na kinzani za kijamii zilizojitokeza hivi karibuni nchini humo na hivyo kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe uliosomwa kwa niaba yake na Askofu mkuu Aldo Giordano, Balozi wa Vatican nchini Venezuela, anasema kwamba, anawasindikiza katika sala na sadaka yake, ili amani, upatanisho na umoja wa kitaifa viweze kutawala tena. Anatambua shida na mahangaiko ya wananchi wengi wa Venezuela na kwamba, wote hawa anawakumbuka kwa kusema kwamba, machafuko na ghasia kamwe hayawezi kuleta, amani, ustawi na maendeleo ya watu.

Majadiliano ya kina yawasaidie kugundua na kuthamini mambo msingi yanayowaunganisha, ili kuweza kupata ufumbuzi wa mgogoro na machafuko ya kisiasa yanayoendelea nchini Venezuela. Uzalendo uwe ni nyenzo msingi itakayowawezesha wananchi wa Venezuela kupambana kikamilifu na athari za myumbo wa uchumi kimataifa, uhalifu na machafuko ya kijamii. Amani na mafao ya wengi yapewe msukumo wa pekee, kwa kuongozwa na imani, utu na heshima ya binadamu.

Baba Mtakatifu anawahimiza wananchi wa Venezuela kujenga na kuimarisha utamaduni wa kukutana na kujadiliana, kwa kutambua kwamba, umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu. Majadiliano haya yawe ni changamoto itakayowawezesha kuwa kweli ni wajenzi wa amani, kwa kuheshimiana na kuthaminiana; kwa kusameheana na kuonjesha huruma kama njia ya kuondokana na falsafa ya chuki na hali ya kulipizana kisasi.

Kwa mwelekeo huu, wataweza kuanza kutembea katika njia mpya, ambayo kimsingi ni ngumu na ndefu, lakini itakayowafikisha kwenye bandari ya amani na haki. Baba Mtakatifu Francisko anawataka viongozi wa Serikali ya Venezuela na vyama vya upinzani kuwa na ujasiri unaojikita katika mafao ya wengi.







All the contents on this site are copyrighted ©.