2014-04-11 16:11:58

Lindeni na kutetea zawadi ya uhai kwa ujasiri na upendo mkuu


Baba Mtakatifu Francisko anawashukuru wajumbe wa Chama cha Maisha nchini Italia kwa kuonesha ukarimu na mshikamano wa pekee ambao umesaidia katika kipindi cha miaka ishirini kuokoa maisha ya watoto ambao pengine wasingebahatika kuona mwanga wa jua. Ni Chama ambacho kimekuwa mstari wa mbele kulinda na kutetea uhai tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake hadi mauti ya kawaida inapomfika kadiri ya mapenzi ya Mungu.

Baba Mtakatifu Francisko ameyasema hayo, Ijumaa, tarehe 11 Aprili 2014 alipokutana na kuzungumza na wanachama wa Chama cha Maisha nchini Italia. Anasema, maisha ya mwanadamu ni matakatifu na yanapaswa kuheshimiwa na kulindwa ni haki msingi ya kibinadamu, ambayo inafumbata haki nyingine zote na wala haifungwi na hali, ubora, au siasa.

Amri ya Mungu inayosema usiue inatetea zawadi ya uhai, changamoto kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kukataa kukumbatia uchumi unaowatenga na kuwaua watu; uchumi unaompima mwanadamu kwa mizani ya bidhaa, hali inayoonesha utamaduni usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine, kiasi cha kuendeleza mchezo huu mchafu katika uhai wa mwanadamu.

Baba Mtakatifu anasema hatari kubwa inayomkumbwa mwanadamu katika ulimwengu mamboleo ni tatizo la kutenganisha uchumi na kanuni maadili; uwepo wa soko huria linaoongozwa na nguvu ya soko pamoja na mabadiliko ya kiteknolojia. Kanuni maadili si jambo linalopewa msukumo wa pekee kama dira na mwongozo wa shughuli za kiuchumi. Hii ni changamoto kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kusimama kidete kulinda na kutetea zawadi ya uhai, tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake, hadi mauti ya kawaida yanapomfika.

Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wanakumbusha kwamba, uhai ukishatungwa, lazima uhifadhiwe kwa juhudi kubwa; kwa hiyo kuharibu mimba na kuwauwa watoto ni mauaji ya kuchukiza kabisa. Wakristo wanachangamotishwa kuwa ni mashahidi wa wa Kiinjili kwa kutetea na kulinda zawadi ya uhai kwa ujasiri na upendo mkuu katika hatua zake zote.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuwa karibu na wanawake wenye shida na mahangaiko yao ya ndani; kwa kuwaheshimu, kuwasikiliza, kuwapokea na kuwasindikiza katika utume wao.







All the contents on this site are copyrighted ©.