2014-04-10 07:44:33

Mikakati ya kupambana na biashara haramu ya binadamu!


Kardinali Vincent Gerard Nichols, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Westenster, Uingereza anasema, ushirikiano kati ya vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na watawa umesaidia kwa kiasi kikubwa kupambana na wimbi la biashara haramu ya binadamu na matokeo yake yanajionesha katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni. Uzoefu na mang'amuzi haya yanaweza pia kutumiwa na nchi mbali mbali duniani katika mapambano dhidi ya biashara haramu ya binadamu inayoendelea kukua na kupanuka siku hadi siku.

Kardinali Nichols ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza na Wales ameyasema hayo wakati alipokuwa anaratibu mkutano wa Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza na Wales kuhusu mbinu mkakati wa kupambana na biashara haramu ya binadamu: Kanisa, utawala wa sheria na ushirikiano". Taasisi ya Kipapa ya Sayansi, inaendesha mkutano huu mjini Vatican kwa kuendelea kuifanyia kazi changamoto iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko ambaye amekuwa akilaani biashara haramu ya binadamu ambayo kwa sasa inaonekana kushika kasi ya ajabu.

Takwimu zinaonesha kwamba, kuna zaidi ya watu millioni mbili na nusu ambao wametumbukizwa katika biashara haramu ya binadamu. Shirika la Kazi Duniani, ILO linasema kwamba, biashara hii chafu inawaingizia wahalifu kiasi cha dolla billioni thelathini na mbili kwa mwaka. Mkutano unaofanyika mjini Vatican unapania pamoja na mambo mengine, kuonesha jinsi ambavyo Vatican kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama sehemu mbali mbali za dunia, inapenda kulivalia njuga tatizo la biashara haramu ya binadamu.

Mkutano huu unawashirikisha wakuu wa ishirini na wawili wa Jeshi la Polisi, kutoka katika Nchi ishirini na mbili pamoja na wakuu wa Europo na Interpol. Kardinali John Olorunfemi Onaiyekan wa Jimbo kuu la Abuja, Nigeria ni kati ya viongozi wa Kanisa wanaochangia, kwani biashara haramu ya binadamu ina madhara makubwa kwa wanawake na watoto wengi kutoka Nigeria. Mkutano huu umewahusisha pia waathirika wa biashara haramu ya binadamu.







All the contents on this site are copyrighted ©.