Jumuiya ya Kimataifa na kamatakamata ya Wasomali nchini Kenya
Jumuiya ya Kimataifa imesikitishwa sana na operesheni kamatakamata iliyofanywa na
Serikali ya Kenya dhidi ya Wakimbizi kutoka Somalia kama sehemu ya mkakati wa kulinda
na kudumisha amani na utulivu dhidi ya mashambulizi yanayofanywa na vikundi vya kigaidi
nchini Kenya.
Serikali ya Kenya kwa upande wake imeeleza kwamba, operesheni
hii inalenga kuvunja nguvu za vikundi vya kigaidi ambavyo vimeendelea kutishia amani
na usalama wa wananchi wa Kenya kwa siku za hivi karibuni, kiasi kwamba, wananchi
hawana tena na uhakika wa usalama wa maisha na mali zao. Walengwa wakuu ni Kikundi
cha kigaidi cha Al Shabaab, ambacho kimepelekea watu kadhaa wakiwemo wanawake na watoto
kukamatwa na kuwekwa kwenye uwanja wa mpira. Taarifa hizi zimethibitishwa na Kamanda
mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Kenya Bwana Benson Kibue.
Shirika la kuhudumia
Wakimbizi la Umoja wa Mataifa linasema, limejitahidi kushauri utoaji wa huduma kwa
wakimbizi na wafungwa wa kisiasa wanaotaka kupata hifadhi ya kisiasa, nchini Kenya
lakini bila mafanikio. Jumuiya ya Kimataifa inaitaka Serikali ya Kenya kuzingatia
na kuheshimu sheria za kimataifa na kwamba, watu waliokamatwa wanapaswa kutendea kama
binadamu na wala si kubaguliwa.