Biashara haramu ya binadamu ni janga na uhalifu dhidi ya ubinadamu!
Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, tarehe 10 Aprili 2014 amekutana na kuzungumza
na washiriki wa mkutano wa pili wa mapambano dhidi ya biashara haramu ya binadamu
ulioandaliwa mjini Vatican na Taasisi ya Kipapa ya Sayansi. Baba Mtakatifu anasema,
biashara haramu ya binadamu ni janga katika maisha ya mwanadamu wa leo, ni uhalifu
dhidi ya binadamu.
Baba Mtakatifu anasema kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa
kuunganisha nguvu zake, ili kuibua mbinu mkakati, weledi na ujuzi kwa kuguswa na huruma
ya kiinjili ili kuwasaidia wahanga na hatimaye, kukomesha biashara haramu ya binadamu.
Vikosi vya ulinzi na usalama vinapaswa kutekeleza wajibu wake kwa kuzingatia sheria
pamoja na kushirikiana na wadau mbali mbali, wanaotoa huduma ya kuwapokea na kuwahifadhi
waathirika.
Baba Mtakatifu anawaalika wadau kujadiliana, kushirikishana na
hatimaye, kukamilishana katika mchakato wa mapambano dhidi ya biashara haramu ya binadamu,
kumbe mikutano kama hii ni ya maana na ni muhimu sana. Baba Mtakatifu anawashukuru
wadau kwa kushirikiana na kufanya kazi kwa pamoja, anawatakia kheri na mafanikio mema
katika shughuli zao.