Papa anahitaji kupata ushauri kutoka kwa Maaskofu wenzake
Papa Paulo VI kunako tarehe 15 Septemba 1965, baada ya kusoma alama za nyakati na
kutambua mahitaji ya Kanisa, akaamua kwa ujasiri mkubwa kuimarisha umoja na mshikamano
kati ya Khalifa wa Mtakatifu Petro na Maaskofu mahalia, waliopewa dhamana ya kuliongoza
Kanisa, akaamua kwa utashi wake mwenyewe kuanzisha Sinodi za Maaskofu, kama chombo
makini cha ushauri kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Sinodi kimsingi ni matunda ya Maadhimisho
ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican.
Tangu wakati huo, Mama Kanisa ameendelea
kuadhimisha Sinodi za Maaskofu ambazo zimetoa mchango mkubwa katika maisha na utume
wa Makanisa mahalia na Kanisa na Kiulimwengu kwa kuangalia fursa, matatizo na changamoto
zinazolikabili Kanisa, ili kutafutiwa ufumbuzi wa pamoja. Sinodi za Maaskofu zimekuwa
ni msaada mkubwa na pia zimetoa ushauri wa kulinda na kuimarisha imani kwa ari, moyo
mkuu na ujasiri katika maisha ya Kikristo sanjari na kuimarisha nidhamu ya maisha
ndani ya Kanisa.
Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili kwa kutambua umuhimu na dhamana
ya Sinodi za Maaskofu, alikwishaona kwamba, kulikuwa na haja ya kufanya maboresho
makubwa katika Maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu, kwa kuongeza mshikamano wa kichungaji
katika Sinodi za Maaskofu. Kumbe, Sinodi za Maaskofu ni mwendelezo wa Fumbo la Kanisa
la Mungu linalojikita katika umoja na utume. Haya ni kati ya mambo yanayopaswa kupewa
msukumo wa pekee kabisa kwa nyakati hizi.
Hivi ndivyo anavyoandika Baba Mtakatifu
Francisko katika barua yake kwa Kardinali Lorenzo Baldisseri, Katibu mkuu wa Sinodi
za Maaskofu, baada ya kufanya uamuzi wa kumpandisha hadhi Monsinyo Fabio Fabene, Katibu
mkuu msaidizi kuwa Askofu. Papa anasema, imekwisha yoyoma takribani miaka hamsini
tangu Sinodi za Maaskofu zilipoanzishwa kwa kusoma alama za nyakati wakati huu anapotekeleza
dhamana na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, anapenda kuonesha mshikamano
wake wa dhati na Maaskofu wote wa Makanisa mahalia kama njia ya kuenzi urithi wa Sinodi
kutoka kwa Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko
anasema katika ukweli na uwazi kwamba, Khalifa wa Mtakatifu Petro anahitaji uwepo
endelevu wa Maaskofu wenzake, ili kupata ushauri, hekima na mang'amuzi, ili wote kwa
pamoja waweze kukiri kwamba, kwa hakika Yesu Kristo ni Mwana wa Mungu aliye hai, sanjari
na kuwa makini kusikiliza sauti ya Roho Mtakatifu kwa ajili ya Kanisa lake. Anawashukuru
wote walioachangia na wale wanaoendelea kuchangia katika kuendeleza na kudumisha Maadhimisho
ya Sinodi za Maaskofu.