Kardinali Lorenzo Baldisseri Katibu mkuu wa Sinodi za Maaskofu anasema, Baba Mtakatifu
Francisko katika Waraka wake wa Kitume Injili ya Furaha, Evangelii Gaudium, EG., ambao
unachota utajiri wake kutoka katika Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu juu ya Uinjilishaji
Mpya iliyofanyika mjini Vatican Oktoba 2012, anawaalika waamini pamoja na watu wote
wenye mapenzi mema kuonja Furaha ya Injili inayotangazwa na Mama Kanisa katika utekelezaji
wa dhamana yake ya Kimissionari sehemu mbali mbali za dunia. Baba Mtakatifu
ametafakari kwa kina na mapana Mapendekezo yaliyotolewa na Mababa wa Sinodi juu ya
Uinjilishaji Mpya, akayachambua na hatimaye akayaingiza kwenye Waraka wake wa Kitume,
Injili ya Furaha. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuwatangazia jirani zao Injili
Furaha. Waraka huu ni matunda pia ya tafakari ya Neno la Mungu, Mafundisho ya Mababa
wa Kanisa na Nyaraka mbali mbali zilizokwishatolewa na watangalizi wake pamoja na
baadhi ya waandishi na wataalimungu wanaogusa changamoto za Uinjilishaji katika ulimwengu
mamboleo. Kardinali Baldisseri anaendelea kubainisha kwamba, Waraka huu unafanya
rejea ya kina mintarafu nyaraka za Mabaraza ya Maaskofu Mahalia na Sinodi za Mapatriaki.
Hapa Baba Mtakatifu anapenda kukazia umuhimu wa Sinodi kama chombo muhimu sana kinachoweza
kumsaidia Khalifa wa Mtakatifu Petro kutekeleza wajibu wake katika maisha na utume
wa Kanisa la kiulimwengu, bila kusahau mchango wa kina unaotolewa na Mabaraza ya Maaskofu
mahalia. Baba Mtakatifu anaitaka Familia ya Mungu kufanya wongofu wa kichungaji, unaojikita
katika asili ya Kanisa linalotumwa kwenda kutangaza Injili ya Furaha. Wongofu wa kichungaji
unamgusa hata Khalifa wa Mtakatifu Petro. Hili ni wazo endelevu kutoka kwa Mababa
wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, ambalo kwa sasa halina budi kufanyiwa kazi kama
kielelezo makini cha umoja na mshikamano wa Kanisa, kama walivyosema Mababa wa Mtaguso
mkuu wa Pili wa Vatican “Collegiality”. Ni suala linalogusa Mafundisho Tanzu ya Kanisa
na Madaraka ndani ya Kanisa. Ni dhana inayokazia umuhimu wa majadiliano ya Kiekumene
na kwamba, Wakatoliki wanayo nafasi ya kujifunza zaidi umuhimu wa umoja na mshikamano
wa kiaskofu na mang’amuzi ya umuhimu wa Sinodi kutoka kwa Makanisa ya Mashariki. Baba
Mtakatifu Francisko yuko makini na anafahamu kile kinachoendelea katika ulimwengu
wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia hususan katika sekta ya elimu,
afya na njia za mawasiliano ya jamii. Katika miaka ya hivi karibuni kumekuwepo na
maendeleo makubwa ya teknolojia ya mawasiliano, kiasi kwamba, ulimwengu kwa sasa unafanana
kama Kijiji. Baba Mtakatifu anatambua fika athari za ulimwengu wa utandawazi na maendeleo
ya sayansi na teknolojia. Watu wanapata mafuriko ya habari na takwimu na kwamba, wote
wanatendewa haki sawa, hali ambayo wakati mwingine inasababisha kinzani na mmong’onyoko
wa tunu msingi za kimaadili. Kutokana na changamoto hizi, anasema Askofu mkuu Claudio
Maria Celli, Rais wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano ya Jamii kwamba, kuna haja ya
kuwa na majiundo makini katika sekta ya elimu yatakayowawezesha watu kuwa na upeo
mpana zaidi katika matumizi ya maendeleo haya kwa kuzingatia tunu msingi za maisha
adili na utu wema. Baba Mtakatifu anawachangamotisha waamini kutoka huko walikojificha
na kuanza hija ya mchakato wa kukutana na watu wengine ili kuwashirikisha Injili ya
Furaha kwa kuishi, kushikamana na kutaabikiana pamoja. Kweli za Kiinjili hazina budi
kuwasilishwa kikamilifu kwa kutambua kwamba, wakati mwingine Kweli za Kiinjili hazipewi
umuhimu na uzito unaostahili. Watangazaji wa Injili wanapaswa kufikisha ujumbe
kwa hadhira inayokusudiwa kwa ufasaha, ili Injili iweze kugusa sakafu ya mioyo ya
watu. Hapa Baba Mtakatifu anawataka Wainjilishaji kujikita katika mambo msingi, yaliyo
mazuri na muhimu; yenye mvuto na mashiko na kwamba, yanafumbata ukweli. Kweli za Kiinjili
ziwafikie watu wa kawaida ili waguswe na kuvutika na Injili ya Furaha, kwani Neno
la Mungu lina nguvu na linatoa hamasa.