Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake, Jumatano tarehe 9 Aprili 2014, kwenye
Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican uliokuwa umefurika kwa umati
mkubwa wa watu, ameanza Katekesi mpya inayofanya tafakari kuhusu karama za Roho Mtakatifu.
Ikumbukwe kwamba, Roho Mtakatifu mwenyewe ni zawadi ya Mungu, inaonesha kwa namna
ya pekee upendo wa Mungu ndani ya Kanisa na katika mioyo ya waamini.
Kwa kuzingatia
unabii uliotolewa na Nabii Isaya, Mama Kanisa katika Mapokeo yake anatambua karama
saba za Roho Mtakatifu: Hekima na Akili; Ushauri na Nguvu; Ufahamu, Maarifa na Uchaji
wa Mungu. Baba Mtakatifu anasema, Hekima ndiyo Karama ya kwanza katika orodha hii.
Hii ni karama ya maisha ya kiroho, ni mwanga wa maisha ya mtu na nuru inayomwezesha
mwamini kutafakari mambo ya kimungu kwa jicho la kimungu kwa moyo wa unyenyekevu kadiri
ya maongozi ya Roho Mtakatifu.
Hekima ni karama inayoibuliwa kwa kuwa karibu
zaidi na Mwenyezi Mungu kwa njia ya sala na mshikamano wa upendo. Ni karama inayomwezesha
mwamini kutambua kwa furaha mpango wa Mungu katika mambo yote. Hekima ya maisha ya
Kikristo ni neema ya Mungu na uwezo wa kutambua uwepo na uzuri wake unaowazunguka
watu wake.
Baba Mtakatifu Francisko anasema, dunia ya leo ina kiu ya kuona
watu wakitolea ushuhuda wa karama hii. Huu ni mwaliko wa kusali ili kumwomba Mwenyezi
Mungu aweze kuwakirimia waja wake karama hii, ili kwa kufurahia katika Roho Mtakatifu,
waamini wanaweza kuwa kweli ni watu wa Mungu; wakiwa wazi kwa hekima na nguvu ya upendo
wake unaokoa.
Baba Mtakatifu anawataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema
kuhakikisha kwamba, wanayapatia maisha yao ladha ya uwepo wa Mungu, kwa njia ya Roho
Mtakatifu waweze kung'amua mema na mabaya; kwa kumtambua Mungu katika yote kwa kuwaonjesha
wengine upendo na huruma yake. Anawataka waamini kukua na kukomaa katika hekima ya
Kimungu, ili waweze kuwa kweli ni wataalam wa mambo ya Kimungu kwa kuwashirikisha
jirani zao.
Baba Mtakatifu anasema, Roho Mtakatifu anawafundisha waamini na
kuwapatia hekima na Ukweli wa Kristo. Huu ni mwaliko wa kumkimbilia mara kwa mara
ili waamini hao waweze kuwa ni Wafuasi kweli wa Yesu Kristo. Kipindi hiki cha Kwaresima
ni fursa ya kumwomba Mungu msamaha kwa kushiriki kikamilifu katika Sakramenti ya Upatanisho.
Wagonjwa waunganishe mateso na mahangaiko yao katika Msalaba wa Kristo; wanandoa wasameheane
na kusaidiana wao kwa wao.