2014-04-09 09:09:58

Jumuiya ndogo ndogo za kikristo ni chombo cha Uinjilishaji Mpya


Baraza la Maaskofu Katoliki Korea linaendelea kujiandaa kikamilifu kwa ajili ya hija ya kichungaji ya Baba Mtakatifu Francisko nchini humo mwezi Agosti, 2014, kama sehemu ya Maadhimisho ya Siku ya Vijana Barani Asia. Katika mwelekeo huu, Maaskofu wamechapisha mwongozo utakaoisaida Familia ya Mungu nchini Korea kutambua moyo, sheria na kanuni; uzoefu na mang'amuzi ya Jumuiya Ndogo ndogo za Kikristo mintarafu changamoto za mikakati ya shughuli za kichungaji sanjari na utekelezaji wa Uinjilishaji Mpya.

Jumuiya ndogo za Kikristo ni shule ya Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa, Maisha adili, upendo na mshikamano wa kidugu. Nchini Korea, Jumuiya hizi zilianza kushika kasi kunako miaka 1990 na kwamba, matunda yake yamekuwa ni kikolezo kikuu katika kukabiliana na changamoto za Uinjilishaji Mpya katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia, nchini Korea na Asia katika ujumla wake. Uimarishaji wa Jumuiya Ndogo ndogo za Kikristo wanasema Maaskofu Katoliki Korea ni kutaka kujenga mshikamano wa dhati miongoni mwa Familia ya Mungu.

Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo zimepata umaarufu mkubwa Amerika ya Kusini na Barani Afrika, hususan katika Nchi za AMECEA ambako zinapewa kipaumbele cha pekee kama sehemu mbinu mkakati wa shughuli za kichungaji, zinazopania Uinjilishaji wa kina, unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo zimekuwa kweli ni vitalu vya sala, tafakari ya Neno la Mungu linalomwilishwa katika matendo ya huruma.

Ni nyenzo muhimu sana katika Uinjilishaji mpya hata katika azma ya kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wa maisha unaotolewa na waamini walei. Nchini Korea, kwa takribani miaka ishirini, Maaskofu wameendelea kuanzisha na kuimarisha Jumuiya Ndogo ndogo za Kikristo kama sehemu ya mikakati ya shughuli za kichungaji kwa Kanisa nchini Korea.

Waamini nchini Korea wanaendelea kusubiri kwa hamu hija ya kichungaji itakayofanywa na Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 14 hadi tarehe 18 Agosti 2014.







All the contents on this site are copyrighted ©.