2014-04-09 11:44:23

Huduma ya Mashemasi isindikizwe kwa sala na mashauri ya Kiinjili


Umati mkubwa wa Familia ya Mungu kutoka sehemu mbali mbali za dunia, Jumamosi, tarehe 5 Aprili 2014, ulishuhudia Majandokasisi kumi na mmoja kutoka Shirika la Bikira Maria wa Mlima Karmeli wakipewa Daraja Takatifu la Usemasi wa Mpito katika Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Askofu Anders Arbolieus kutoka Jimbo Katoliki la Stockholm, Sweden, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Pancras, Roma.

Askofu Anders anasema, Kanisa lilikuwa na kila sababu ya kumshukuru Mungu kwa kuliwezesha kupata Mashemasi wapya kumi na mmoja, kwani hawa ni matunda ya mbegu ya miito mitakatifu iliyopandwa ndani ya Kanisa na sasa inaanza kuzaa matunda, ambayo ni sehemu ya furaha ya Pasaka ya Kristo, hata kama bado Kanisa linaendelea na hija ya Kipindi cha Kwaresima.

Askofu Anders anasema, huduma ni dhana inayopaswa kupewa msukumo wa pekee katika maisha na vipaumbele vya watu. Mashemasi wanapaswa kutambua kwamba, wao ni watu wa huduma wanaoongozwa na mwanga wa Kristo mwenyewe aliyekuja kuhudumia na wala si kuhudumiwa na kuyatoa maisha yake, ili yawe ni fidia ya wengi. Hii ndiyo changamoto inayoendelea kutolewa na Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Ushemasi ni Daraja la Huduma inayopaswa kugusa undani wa maisha ya watu, kwani Yesu mwenyewe, alionesha ushuhuda huu kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake. Huduma ya Mashemasi haina budi kujikita katika maisha ya sala na tafakari ya kina, inayomwilishwa katika matendo na maisha adili. Sala iwawezeshe Mashemasi kujenga na kudumisha umoja na Kristo. Wajitahidi kuwasaidia watu kugundua umuhimu wa maisha yao kuwa ni wimbo wa sifa na utukufu kwa Mwenyezi Mungu. Waamini wasaidiwe kugundua wito na utume wao wa kinabii kwa kuumwilisha katika mazingira kwa njia ya huduma makini kwa wote wanahitaji msaada wao.

Mashemasi wapya wanachangamotishwa kuwasaidia waamini kuweza kufungua macho ya mioyo yao ili kutambua uwepo endelevu wa Kristo kati yao, mwaliko wa kumtafuta kwa ari na moyo mkuu. Dhana ya huduma ioneshwe kwa kuzunguka Altare, kwani pasi ya huduma, maisha ya Kikristo ni tasa. Kanisa linaweza kupata waamini wengi, ikiwa kama litajielekeza katika huduma makini inayosimikwa katika unyenyekevu na unyofu wa moyo! Kwa njia hii, watu watamwona Kristo kati yao na kuweza kumpokea. Huduma ya Kanisa isindikizwe kwa njia ya Sala na Mashauri ya Kiinjili.

Mashemasi wa Shirika la Bikira Maria wa Mlima Karmeli wanachangamotishwa kuhakikisha kwamba, wanajikita katika umoja na mshikamano kama njia ya kuonjeshana upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo. Kwa njia hii, Mashemasi wanaweza kuwa ni mashahidi hai wa uwepo endelevu wa Kristo kati ya watu wake. Huyu ndiye Kristo aliyekuja kuhudumia kwa kuyamimina maisha yake ili yaweze kuwa ni fidia ya wengi. Askofu Anders Arbolieus amewaomba waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuwasindikiza Mashemasi wapya kwa njia ya Sala na Majitoleo yao.







All the contents on this site are copyrighted ©.