Washeni nyoyo za watu kwa upendo na ukarimu kutoka kwa Yesu na Kanisa lake!
Baba Mtakatifu Francisko amewashukuru wajumbe wa kamati ya Maandalizi ya Maadhimisho
ya Siku ya Vijana Duniani iliyofanyika mjini Rio de Janeiro, Brazil kwa kusema kwamba,
ni hija ya kichungaji ambayo itakuwa vigumu sana kwake kuisahau. Hii ni kutokana
na mapokezi makubwa, ukarimu na majitoleo ya wanachi wa Brazil waliomwonjesha na kumshirikisha,
kiasi kwamba, upendo wa Mungu ukaweza kupenya katika mioyo ya mamillioni ya vijana
waliokuwa wamekusanyika mjini Rio de Janeiro.
Baba Mtakatifu anasema, alipofika
nchini Brazil aliwaomba wananchi wa Brazil kumpokea na kumkaribisha miongoni mwao
na kwamba, aliporejea tena mjini Roma, alibaki na hamu ya kutaka kubaki Brazil. Anawashukuru
wote walioachangia kwa hali na mali katika kufanikisha Maadhimisho ya Siku ya Vijana
Duniani. Kuna watu wamejisadaka, wamekumbana na kinzani, lakini yote yamekwenda vyema
kadiri ya mpango wa Mungu, licha ya mapungufu na ukosefu wa rasilimali.
Hivi
ndivyo Yesu alivyofanya alipowalisha watu elfu tano kwa mikate mitano na samaki wawili,
changamoto ya kusonga mbele kwa imani na matumaini kwa kuendelea kumtegemea Mwenyezi
Mungu. Upendo wa Kristo unawawajibisha waamini kuendelea kuonesha mshikamano na watu
wanaoishi katika mazingira magumu ili waweze kuonja urafiki unaobubujika kutoka kwa
Yesu. Baba Mtakatifu anawataka wanakamati hawa kusonga mbele pasi na woga ili kuwahudumia
watu.
Kanisa linapaswa kujikita katika ari na moyo wa kimissionari ili kuwatangazia
watu Injili ya Furaha pasi na woga wala kujibakiza kwa ajili ya Injili ya Kristo.
Ili kutekeleza wajibu huu, Baba Mtakatifu anawaalika waamini kumwangalia Mtakatifu
Yosefu wa Anchieta, mtume wa Brazil aliyetangazwa hivi karibuni kuwa Mtakatifu anayesema
kwamba, si vigumu kwa wale wanaowafaraji wengine wakiwa na lengo la kuonesha utukufu
wa Mungu na wokovu wa roho za watu, kiasi hata cha kuthubutu kutoa maisha yao.
Baba
Mtakatifu anawaalika wajumbe wa Kamati ya Maandalizi ya Siku ya Vijana Duniani nchini
Brazil kusonga mbele kwa furaha na ujasiri wa kuwasha nyoyo za wananchi wa Brazil
kwa upendo wa Yesu na Kanisa lake.