Ujumbe wa Papa Francisko kwa Maaskofu Katoliki Tanzania
Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 7 Aprili 2014 amekutana na kuzungumza na
Maaskofu Katoliki Tanzania ambao wako kwenye hija ya kitume mjini Vatican kama kielelezo
cha kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Anasema,
Kanisa la Tanzania limebahatika kuwa na historia inayojikita katika dhana ya Umissionari,
inayowasukuma watoto wa Kanisa kujitosa kimasomaso kuwatangazia wengine Injili ya
Furaha.
Hii ni changamoto ya kuhakikisha kwamba, Kanisa la Tanzania linakuza
ari na mwamko wa Kimissionari, ili kweli za Kiinjili ziweze kupenya katika medani
mbali mbali za maisha, ili kuandika ukurasa mpya wa historia ya Uinjilishaji nchini
Tanzania. Uinjilishaji bado unaendelea kujionesha nchini Tanzania katika maisha na
utume wa Kanisa; katika maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa, maisha ya kisakramenti,
mchango wa Kanisa katika sekta ya elimu na afya, Katekesi na maisha ya kawaida ya
Wakristo.
Huu ni mwaliko kwa waamini kutolea ushuhuda wa maisha yao kwa kumtangaza
Yesu Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu. Hii ndiyo changamoto
kubwa anasema Baba Mtakatifu kwa wakristo nchini Tanzania, kuhakikisha kwamba, wanakuwa
ni mashuhuda wa upendo wa Kristo unaomkomboa mwanadamu, kwa kumwilishwa na kuadhimishwa
na waamini ndani ya Kanisa.
Baba Mtakatifu Francisko analishukuru Kanisa Katoliki
Tanzania kwa kuendelea kutolea ushuhuda wa kimissionari kwa kuwahudumia wagonjwa wa
Ukimwi pamoja na kuwajengea uwezo wa kupambana na Ukimwi kwa kuwajibika barabara na
kudumisha maadili mema. Analishukuru Kanisa kwa kujikita katika maendeleo ya mtu mzima:
kiroho na kimwili. Baba Mtakatifu anawaombea Wakristo nguvu, hekima na utakatifu wa
Wamissionari wa kwanza uendelee kulihamaisha Kanisa kuwa kweli ni kielelezo cha ushuhuda
wa Kristo na Kanisa lake.
Baba Mtakatifu anasema, ili Kanisa liweze kweli kutekeleza
utume wake wa: kufundisha, kutakatifuza na kuongoza, linawahaitaji Mapadre wasomi,
wema na watakatifu; ni watu wanaohitaji kupatiwa majiundo makini ya awali na endelevu:
kiutu, kiroho, kiakili na kichungaji, ili waweze kuendelea kuwa kweli ni watumishi
waaminifu kwa ahadi walizoweka wakati walipopokea Sakramenti ya Daraja Takatifu. Majiundo
endelevu yajikite katika wongofu na upendo katika shughuli za kichungaji na kwa njia
hii wanaweza kuwa kweli ni vyombo vya mageuzi ya maisha ya kiroho katika Parokia kwa
kuonesha umoja na mshikamano; kivutio kikuu kwa vijana wanaotaka kujitosa ili kumtumikia
Kristo na Kanisa lake kwa njia ya Daraja Takatifu la Upadre.
Baba Mtakatifu
Francisko anaendelea kuhimiza dhamana na ushiriki wa waamini walei katika maisha na
utume wa Kanisa kama ilivyojionesha na kusisitiziwa kwenye Kongamano la Ekaristi Takatifu
Kitaifa lililofanyika kunako Mwaka 2012 pamoja na Maadhimisho ya Mwaka wa Imani. Haya
ni matukio muhimu katika kukuza na kuimarisha imani ya Watu wa Mungu nchini Tanzania.
Makatekista wanapaswa kupongezwa zaidi kwa kuwatangazia jirani zao Injili pamoja na
kuwashirikisha utimilifu wa maisha na mafundisho ya Kikristo.
Baba Mtakatifu
anasema, hizi ni nyenzo msingi katika kupambana na imani za kishirikina, madhehebu
yenye misimamo mikali pamoja na mawazo mepesi mepesi, lakini jambo la msingi ni kuhakikisha
kwamba, waamini wanashirikisha vijana uzuri na utajiri wa imani ya Kanisa Katoliki.
Kila mwamini awe ni chachu ya kuleta mabadiliko ndani ya Jamii na kwamba, waamini
walei waliofundwa barabara wanaweza kuwa ni vielelezo vya utu na maadili mema katika
tamaduni na kazi za watu, changamoto endelevu kwa nyakati hizi.
Baba Mtakatifu
Francisko katika hotuba yake kwa Maaskofu Katoliki Tanzania amekazia pia umuhimu wa
kuendelea kuinjilisha Familia, kwa kutambua kwamba, hiki ni kiini cha Uinjilishaji
Mpya kama wanavyokazia Mababa wa Sinodi Maalum ya Maaskofu iliyofanyika kunako Mwaka
2009. Familia zijengewe moyo na ari ya kusali, uaminifu katika maisha ya ndoa ya mke
mmoja, usafi wa roho na unyenyekevu katika huduma, kwa kutambua kwamba, Kanisa Katoliki
nchini Tanzania linaendelea kuchangia katika ustawi na mafao ya wengi katika sekta
ya elimu na afya, mambo msingi katika ujenzi wa utulivu na maendeleo ya nchi.
Kanisa
lisimame kidete kushuhudia utakatifu wa maisha ambayo ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi
Mungu, dhamana inayoweza kuendelezwa na familia thabiti kama sehemu ya mchakato wa
kuwaandaa vijana wa kizazi kipya ili kukabiliana na changamoto za maisha kwa: hekima,
ujasiri na ukarimu.
Baba Mtakatifu Francisko anasema, anaridhishwa na jitihada
zinazofanywa nchini Tanzania kuhakikisha kwamba kuna kuwepo na uhuru wa kuabudu; kwa
kuheshimu na kuzingatia haki msingi za binadamu; uhuru wa dhamiri nyofu sanjari na
kuheshimu utu wa mwandamu. Yote haya yanapania umoja wa kitaifa, amani na mafao ya
wengi.
Baba Mtakatifu analipongeza Kanisa Katoliki Tanzania kwa kuendeleza
mchakato wa msamaha, amani na majadiliano kati ya watanzania ambao kwa wakati mwingine
wanakabiliana na madhulumu na matumizi ya nguvu. Umoja na mshikamano katika maisha
na sala ni nguvu thabiti katika kukabiliana na changamoto hizi pamoja na kuonesha
dira inayopaswa kufuatwa na Jamii.
Baba Mtakatifu anawahamasisha Maaskofu
kushirikiana na Serikali pamoja na vyama vya kiraia, ili kuhakikisha kwamba, utawala
wa sheria unazingatiwa kama njia ya ujenzi wa Jamii inayosimikwa katika haki na amani
katika kutatua migogoro mbali mbali ya kijamii ili kudumisha amani.
Imeandaliwa
na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.