2014-04-07 10:30:49

Papa atembelea Parokia ya Mtakatifu Gregorio Magno, Roma!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili jioni, tarehe 6 Aprili 2014 alitembelea pamoja na kuadhimisha Ibada ya Misa takatifu kwenye Parokia ya Gregorio Magno, iliyoko Jimbo kuu la Roma. Katika mahubiri yake, Baba Mtakatifu amekazia umuhimu wa imani katika ufufuko wa wafu na kwamba, kila mwamini katika maisha yake, kuna sehemu ambayo imekufa, hiki ni kifo cha maisha ya kiroho, changamoto na mwaliko wa kumkaribisha Kristo ili aweze kuwaletea uponyaji wa ndani, kama alivyofanya kwa rafiki yake Lazaro.

Baba Mtakatifu anasema, waamini wanaendelea kuogelea katika dimbwi la dhambi, ubinafsi pamoja na kukumbatia maisha ya giza, rushwa na ufisadi; mambo ambayo yanaleta kichefuchefu kwa kutoa harufu mbaya kama alivyosema Martha, dada yake Lazaro. Kwaresima ni kipindi cha kusikiliza tena kwa makini, sauti ya Yesu inayomwita kila mwamini kutoka katika kaburi la maisha yake ya kiroho, tayari kutembea katika mwanga, upendo, huruma na msamaha unaotolewa na Kristo mwenyewe, ili kuonja tena maisha mapya.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini wote kujishikamanisha na Kristo, ili aweze kuwaondoa katika makaburi yao. Jumapili ya tano ya Kwaresima ni kipindi maalum kwa ajili ya Wakatekumeni kupokea Neno la Mungu. Akiwa Parokiani hapo, Baba Mtakatifu amewagawia waamini Biblia ndogo ndogo wanazopaswa kutembea nazo, kuzisoma, kutafakari na hatimaye, kumwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha yao. Iwe ni fursa pia ya kujiandaa kusherehekea Pasaka ya Bwana.

Baada ya Ibada ya Misa Takatifu, Papa Francisko alipata nafasi ya kukutana na makundi mbali mbali. Baba Mtakatifu anawakumbusha waamini kwamba, mahali muafaka pa kuweza kukutana na kuzungumza na Yesu ni katika udhaifu na mapungufu ya mtu mwenyewe. Ni mwaliko wa kwenda pembezoni mwa maisha ya kila mtu, ili kuonja kweli uwepo wa Yesu Kristo, Neno wa Mungu aliyefanyika mwili, akateswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu, changamoto ya kumwamini kwa dhati.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini kujenga na kudumisha utamaduni wa upendo na mshikamano kwa kukumbatia Injili ya uhai ili kuondokana na utamaduni wa kifo unaoendelea kusababisha mauaji ya watu wasiokuwa na hatia. Mshikamano kwa watu wasiokuwa na fursa za ajira, kielelezo makini cha utu na heshima ya binadamu. Kuna haja ya kuibua sera na mbinu makini zitakazowasaidia vijana kupata fursa za ajira, kwa kujenga utamaduni wa mshikamano. Baba Mtakatifu anawataka vijana kutokata tamaa katika mapambano ya maisha.

Baba Mtakatifu amewapongeza watoto na vijana walionesha kwa njia ya michoro matumaini katika maisha, licha ya shida na magonjwa mbali mbali wanayokabiliana nayo, kwani matumaini kamwe hayawezi kumdanganya mtu. Matumaini ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Baba Mtakatifu anawashukuru wazazi na walezi wanaothubutu kuwapeleka watoto wao ili waweze kubatizwa katika Kanisa, lakini wakumbuke kwamba, wanapaswa kuwasindikiza watoto wao katika safari ya maisha ya Kikristo kwa kuhakikisha kwamba, wanapokea pia Sakramenti nyingine za Kanisa pamoja na kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa.

Akizungumza na wagonjwa pamoja na wazee wa Parokia ya Mtakatifu Gregorio Magno, Baba Mtakatifu amewaomba wagonjwa na wazee kutolea maumivu yao kama sadaka safi na kielelezo cha ushiriki wao katika mateso ya Kristo, kwa ajili ya ukombozi wa dunia. Baba Mtakatifu anawaalika kuendelea kusali kwa ajili ya watu waliokata tamaa ya maisha, ili waweze kutubu na kumwongokea tena Yesu. Baba Mtakatifu anaendelea kuwaomba waamini kumsindikiza kwa njia ya sala katika maisha na utume wake.All the contents on this site are copyrighted ©.