Mwachieni nafasi Kristo ili afungue makaburi ya mioyo yenu!
Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Tafakari ya Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili
tarehe 6 Aprili 2014 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican
anasema kwamba, ufufuko wa Lazaro lilikuwa ni tukio kuu kabisa lililofanywa na Yesu,
ili kuwaimarisha wafuasi wake katika imani katika Fumbo la Mateso, kifo na ufufuko
wake.
Baba Mtakatifu anasema hata leo hii Yesu bado anaendelea kuwalilia wale
wanaoteseka katika kifo na dhambi, ili aweze kuwaonjesha huruma na upendo wake usiokuwa
na kifani. Yesu anawaita waamini kutoka katika maisha ya dhambi, katika ubinafsi na
anasa, ili waweze kuonja uhuru wa kweli pasi na kiburi. ufufuko wa mwamini unaanza
pale anapoonesha utii kwa Yesu, ili kukimbilia mwanga na maisha mapya, kwa kutambua
kwamba, wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.
Baba Mtakatifu anasema, huu
ni mwaliko wa kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu, kwani huruma yake haina mipaka.
Yesu yuko tayari kutoa jiwe kwenye kaburi la maisha ya waamini; jambo linalowatenganisha
na Kristo.