2014-04-07 10:22:12

Miaka 20 tangu yalipotokea mauaji ya kimbari nchini Rwanda


Tarehe 7 Aprili 2014, Rwanda inafanya kumbu kumbu ya miaka ishirini, tangu mauaji ya kimbari yaliyopokea nchini humo na kusababisha maafa makubwa kwa watu wasiokuwa na hatia, kunako Mwaka 1994. Baba Mtakatifu Francisko, wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili iliyopita kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro Mjini Vatican, amelikumbuka tukio hili, kwa kuonesha uwepo wake wa karibu kwa njia ya maisha ya kiroho.

Papa ametaka Wanyarwanda wote kusonga mbele kwa imani na matumaini, katika mchakato wa upatanisho, ambao tayari unaanza kuonesha matunda makubwa. Hii ni changamoto ya kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano wa kiutu na maisha ya kiroho, kwa ajili ya ustawi na mafao ya wananchi wote wa Rwanda. Baba Mtakatifu anawaalika wananchi wote wa Rwanda kutokuwa na woga, bali wajishikamanishe na kujenga nchi yao katika misingi na kweli za Kiinjili, katika upendo na maridhiano, ili amani ya kweli iweze kupatikana.

Baba Mtakatifu Francisko amewaombea ulinzi na tunza ya kimama kutoka kwa Bikira Maria wa Kibeho. Anawakumbuka Maaskofu Katoliki Rwanda waliohitimisha hija yao ya kitume hapa mjini Vatican hivi karibuni.

Baba Mtakatifu amewakumbuka pia waathirika wa ugonjwa wa Ebola huko Guinea na nchi jirani ambako zaidi ya watu themanini tayari wamekwisha poteza maisha yao

Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko amewagawia Biblia Takatifu, waamini waliokuwa wamefurika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, kama kielelezo cha kuwakabidhi Waketekumeni Neno la Mungu ili waweze kujiandaa barabara katika Maadhimisho ya Fumbo la Pasaka.







All the contents on this site are copyrighted ©.