Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, Jumapili
iliyopita, tarehe 6 Aprili 2014 kwa kushirikiana na Maaskofu Katoliki Tanzania ambao
wako katika hija yao ya kitume mjini Vatican, wameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu
kwenye Parokia ya Bikira Maria wa Salette, Kanisa la Kitume la Kardinali Polycarp
Pengo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam. Ibada hii imehudhuriwa na umati
mkubwa wa Makleri, Watawa, Waamini walei pamoja na Wanaparokia ili kuonesha kwamba:
Kanisa ni: Moja, Takatifu, Katoliki na la Mitume.
Mahubiri yalitolewa
na Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwaichi wa Jimbo kuu la Mwanza aliyekazia umuhimu wa
kutubu na kumwongokea Mungu hasa katika kipindi hiki cha Kwaresima, kama sehemu ya
maandalizi ya Maadhimisho ya Fumbo la Pasaka. Neno la Mungu liwe ni mwongozo na dira
ya maisha ya waamini kwa kulimwilisha katika uhalisia wa maisha, ili aweze kuwa kweli
huru na kifo, dhambi pamoja na mambo yote yanayomtumbukiza katika giza na ulevegu
wa maisha ya kiroho.
Kwa njia ya Fumbo la Pasaka, waamini wawe huru kuchuchumilia
tunu ya maisha mapya kwa kuepuka kuendelea kuwa wahanga wa dhambi na mauti, kwa kupenda
kutembea kama watu huru katika njia za Bwana, pasi na kukata tamaa ya kifo, daima
wakijitahidi kumrudia Mungu, ambaye ni mwingi wa huruma na mapendo.
Mwanadamu
anaendelea kuandamwa na magonjwa, kifo na maziko kama ilivyokuwa kwa Lazaro anayeimuliwa
katika Injili ya Jumapili ya tano ya Kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka A wa Kanisa.
Yesu kama rafiki mwaminifu wa binadamu anaendelea kuwatembelea binadamu katika shida
na mahangaiko yao kama alivyofanya kwa Rafiki yake Lazaro, kwani anawapenda na anataka
kuwaokoa na kuwakirimia mwanga unaopaswa kupokelewa na kuthaminiwa. Yesu anataka kuwapatia
rafiki zake ufufuko na maisha mapya yanayojikita katimka imani, matumaini na mapendo.
Ibada ya Misa Takatifu ilipambwa kwa nyimbo za Kwaresima zilizoimbwa vizuri
na Watawa, Makleri na Waamini walei, waliokuwa wanasindikizwa kwa kinanda kilichokuwa
kinatekenywa kwa ufundi na utaalam mkubwa kutoka kwa Padre Alcuin Nyirenda, OSB, hapa
Waswahili wakasema, ama kweli, leo upele ulipata mkunaji! yaliyojiri baadaye, usikose
kujiunga nasi tena, tutakapoendelea kukuchambulia kwa kina na mapana, hija ya kitume
ya Maaskofu Katoliki Tanzania hapa mjini Vatican.
Imeandaliwa na Padre
Richard A. Mjigwa, C.PP.S Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.