2014-04-05 06:52:04

Usilete mzaha, ananuka!


Manamuziki Remmy Ongala anakilalamikia kifo pasipo kutushauri tukikabilije: “kifo kifo kifo hakina huruma! Ukitaka kujua ubaya wa kifo, pita hospitalini, utakuta wengine wanalia. Wengine hawana miguu tena, wengine wana vidonda, wengine wana vipele, wengine wana ukurutu, wengine wamezaa watoto wamekufa shauri yako wewe kifo, kifo kwa nini unatusumbua. Tumezaliwa shauri ya kuishi. Ulimwengu bila watu siyo ulimwengu tena. Kifo we! Kifo kifo kifo hakina huruma…. Kifo ni kiboko yao!” RealAudioMP3

Ni ukweli kabisa, kifo hakina huruma, kifo kinatia uchungu, kifo kinakatisha tamaa ya maisha. Mbele ya kifo watu tunalia machozi. Ongala anakilaani kifo kiasi kwamba anaona hata magonjwa na ajali yanasababishwa na kifo. Ninakipongeza kifo kwa sababu kinatufanya watu wote tulingane! Kinamvaa kila mtu, bila kujali umri, cheo, ukuu, kabila, dini, jinsia. Kifo hakipokei rushwa. Ama kweli kifo ni kiboko kikali! Bahati mbaya na nzuri ya kifo kinawafanya wafiwa wengi wachanganyikiwe na kuanza kumlaani na kumtukana Mungu, kwa wafiwa wengine kinawakomaza kiimani na kimaadili. Hata kama tukilia na kulalalmika namna gani kifo kinabaki palepale na msimamo wake! Kifo ni suala nyeti. Je, haiwezekani kufanya appointment ya kukutana na kifo na kujadiliana naye suala hili nyeti?

Jumapili iliyopita tulitafakari “Ishara” jinsi anavyoita Mwinjili Yohana kuhusu uponyi wa upofu. Jinsi kipofu anavyozawadiwa mwanga au anavyofunguka macho. Ishara ile ilikuwa kama aina mpya ya uumbaji anaofanya Kristo. Lakini hata baada ya huko kufunguka macho, tunabakiwa bado na maswali dodoso ya kujihoji juu ya maisha. Mosi, Kristu anatufungua macho ili tuone nini au twende wapi? Pili, je, lengo la kutufungua macho ni kwa ajili ya kuona tu mambo hapa duniani halafu mwisho wake iwe nini?

Aidha, hata kama Yesu ananifungua macho na kuniwezesha kutembea vyema humu ulimwenguni, Je, maisha haya yana maana gani endapo hayana hatima? Je uzee usioisha na unaoendelea tu bila kwisha utauita ni ushindi dhidi ya kifo? Halafu hali hiyo ya uzee itaishia wapi wakati ulimwengu unaendelea kudumu tu hata bila ya mimi? Je, maisha hayo yanayoendelea tu yatakuwa na maana gani ndani yangu? Maswali kama haya ndiyo tutakayoyatafakari katika injili ya leo.

Tukitaka kuelewa vizuri hali halisi ya maisha tunayoyaishi, hatuna budi kuangalia kwa makini upi ni mwisho wake. Ni sawa na usafiri wa mguu usianze tu kusafiri kichwakichwa bila kujua wapi unaenda na umbali wake. Tunaposema mwisho wa maisha tunamaanisha kifo. Yaani, yabidi kukitafakari kifo, vinginevyo maisha yetu yote yanakuwa ni kutorokatoroka na kukikimbikimbia kifo, kwa kuogopa kukabili ukweli huo wa maisha ambao hatuna budi kuukabili.

Ni utamaduni wa binadamu ambao mara nyingi matendo ya maisha yetu yanajaribu kuepa kupanga ratiba ya kukutana na kifo. Kumbe, unaona kifo kinaendelea kututia wazimu hadi kutukosesha raha kabisa. Muziki wa Ongala unatupa hali halisi ya woga wa binadamu mbele ya kifo. Ni woga mkuu usioleta matumaini. Ama kweli “usilolijua litakusumbua.”

Ni ukweli dhahiri kwamba sisi binadamu tumeumbwa kwa ajili ya maisha ambayo hayana kikomo. Kwa hiyo ni vyema kukumbuka maneno ya mzaburi anayosema: “Ee Bwana utufundishe kuhesabu siku zetu, tujipatie hekima ya moyo” (Zab. 90:12). Tuwe na busara kutambua siyo kwa woga kwamba maisha yetu ni mafupi sana na tujaribu kuyapangilia vizuri.

Leo tumebahatika kuwa na mihadi (appointment) ya majadiliano na kifo kilichomwingia mwenzetu Lazaro. Msemaji mkuu katika mazungumzo hayo ni Yesu pamoja na wafiwa ambao ni dada wa damu wa mfu.

Tukifuatilia kwa makini mazungumzo hayo tutagundua uhondo uliomo katika ishara hiyo na kuelewa kifo ni nini na kina faida au hasara gani kwetu. Awali ya yote tuelewane juu ya matumizi ya msamiati wa neno kufufuka na tunavyolitumia kwa Lazaro. Hilo neno hapa siyo pahala pake kwa sababu neno kufufuka linamaanisha hali ya kupita toka ulimwengu huu na kuingia mbinguni kwenye maisha ya milele ya kukaa na Mungu Baba. Kwa mfano tunazungumza juu ya kufufuka kwa Yesu ikiwa na maana kwamba ameingia mbinguni na kuketi pamoja na Mungu Baba.

Kwa hiyo Yesu amefufuka yaani amepita toka ulimwengu huu na kuingia ulimwengu wa Baba. Kufika mbinguni na kumwona Mungu ni kikomo komesha na “Hakuna aliyemwona Mungu akarudi tena duniani.” Kwa hiyo kama Yesu alimfufua Lazaro ambaye alishaingia katika ulimwengu wa Baba basi alimkatishia mwenzake uhondo wa kukaa na Mungu. Kwa hiyo tunapozungumzia juu ya Lazaro, tusitumie neno kufufuliwa bali tutumie neno kuhuisha. Lazaro alihuishwa kwa sababu hakuwa ameingia katika maisha ya milele mbinguni.

Lazaro alirudishiwa uhai wake na akaendelea kuishi tena hapa duniani, ingawaje hatujui alikuwa wapi kipindi kile alichokufa na kuzikwa. Kati ya miujiza mingi aliyoyaifanya Yesu tendo hili la kuhuisha lilikuwa la pekee sana kwa watu waliolishuhudia, kwani watu walimwona Lazaro ameshafariki na kunuka. Mwinjili Yohani analichukua tendo hili la Yesu kuwa kama ishara, ili kuonesha jinsi gani Yesu ni Bwana wa maisha haya ya kibiolojia.

Hoja ya Yesu kumrudisha tena Lazaro katika ulimwengu huu wa maisha mapya ambayo hayakuwa yameguswa na aina ile ya maisha yenye malengo, yenye hatima, yaani maisha ambayo hayaishii hapa tu, bali yanaendelea na kuishia kwenye maisha ya Baba wa mbinguni. Huu ndio ujumbe mmojawapo ambao mwinjili anataka kutuletea katika ishara anayoifanya Yesu leo.

Sasa tuione kwa karibu ishara hii ya kuhuishwa kwa Lazaro. Masimulizi yanaanza hivi: “Kulikuwa na mtu aitwaye Lazaro.” Huyu Lazaro, alikuwa mwanafamilia ya namna yake. Kwa sababu katika familia hii hatuwaoni wazazi, yaani baba na mama. Tunaona tu kuna kaka na dada wawili Maria na Marta. Maana yake tunaoneshwa jumuia ya wana ndugu, au tungeweza kusema, jumuia ya kikristu. Jumuia ya kaka na dada ambao yabidi wakabiliane na hali halisi ya maisha. Hali halisi ya maisha tuionayo ni ya homa halafu kifo nk.

Katika familia hii tunasikia kuwa kaka mtu anaumwa homa kali inayopelekea kifo. Kabla mambo hayajawaharibikia, akina dada hawa wanatuma ujumbe kumtaarifu Yesu wakiwa na matumaini kuwa angemponya. Wakamwambia: “Bwana, yeye umpendaye hawezi.” Majibu ya Yesu hayaeleweki kirahisi, anaposema: “Ugonjwa huu si wa mauti, bali ni kwa ajili ya utukufu wa Mungu.” Maana yake, kwa njia ya homa hii kutafumbuliwa kile ambacho Mungu anauwezo nacho na anachotaka kutufundisha. Kwa maneno haya Yesu anataka kusema kwamba yaonekana kuna ugonjwa unaopelekea kifo, na ugonjwa mwingine haupelekei kifo.

Ugonjwa unaopelekea kwenye kifo, ni ule unaoharibu maisha ya kweli ya mtu, yaani maisha yale yasiyo na mwisho. Kama vile isemavyo kwenye kitabu cha Mwanzo. Ukifanya uchaguzi wa mambo kinyume cha yale anayokuagiza Mungu utakufa: “Msile matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya, kwa maana siku utakapokula matunda ya mti huo utakufa hakika.” (Mwa 2:1) Kama hufanyi mambo kadiri alivyoagiza Mungu, unaharibu maisha yako halisi, maisha ya utu, ya binadamu. Huko ndiko kunakoitwa kufa-basi! Lakini kuna homa ambayo inakupeleka kwenye kifo cha kimwili tu (kibaolojia).

Kifo cha kimwili ni kile ambacho Mungu alishakipanga kwa ajili ya binadamu. Kifo cha aina hiyo hatuwezi kamwe kukikwepa. Hiki siyo kifo anachomaanisha Yesu. Ukweli Yesu aliipenda sana familia hii tena ni mapendo ya Kristu yanayotakiwa katika juimuia ya kikristu. Lakini unaona kuwa Yesu anaposikia kwamba Lazaro anaumwa, anabaki alipo na kuchelewa kwa siku mbili zaidi hadi Lazaro anakufa. Je upendo wa Mungu upo wapi pindi anatuacha tufe? Yesu anampenda Lazaro lakini anapomwacha afe anataka kutupa ujumbe. Hapa linaingia suala la ukuu wa Mungu.
Sisi tungependa kwamba Mungu aturuhusu tu tuingie paradisini pasipo kufa. Je, Mungu anaweza kuruhusu jambo hilo? Jibu ni hapana! Mungu angeweza kuruhusu hilo, lakini ingekuwa kama kutudanganya na kutuchanganya, kwamba Mungu anatupatia uhai huu ili aturudishie tena mwili huu wa kibinadamu tuendelee nao bila kwanza kuubadili kidogo. Tatizo ni kwamba, maisha yetu ya kibaolojia, yanahusu ulimwengu huu, lakini kwa vile ndani mwetu tuna maisha ya Kimungu, tunapopaswa kuingia katika maisha ya Mungu, kwa hiyo maisha haya budi yakome. Anayeshiriki maisha ya kimungu hawezi kufa, hawezi kupambana na kifo kile cha kibaolojia. Hadhi yetu ya kibidamu ipo kwa ajili ya kufa ili kuendelea na maisha ambayo Mungu ametuandalia.

Kwa kumwacha Lazaro afe, Yesu anataka kutuonesha waziwazi kwamba yeye hajafika kuzuia kifo hiki cha kibaolojia. Yesu anaacha mambo yafuate mfumo wake wa kimaumbile (wa kibaolojia). Mwanamuziki Mbaraka Mwinshehe anapowalilia wanamuziki waliofariki, anakubali kwamba kifo ni njia ya kila binadamu, anaimba: “Wanamiziki na wanamichezo wote hapa nchini Tanzania, hujiwa na majonzi kila mara tunapowakumbuka waliotutoka. Rambirambi zetu ziwafikie wanandugu. Kifo ni njia ya kila binadamu. Hatuna budi tutoe masikitiko na imani zetu kwa yao mazuri.” Kwa vile “Kifo ni njia ya kila binadamu”, Basi lengo la Yesu likatimia, kwani anapofika Bethania Lazaro alishafariki kitambo na kuzikwa siku nne zimeshapita.

Mandhali anayoikuta Yesu ni ya msiba. Hivi kulikuwa na watu wengi waliofika kuwatuliza wafiwa. Hapa unaalikwa kuvuta taswira (picha) kidogo ya hali halisi inayokuwa msibani, na ya watu wanaotuliza wafiwa. Mara nyingi watuliza wafiwa wanasema: “Poleni na msiba! Mtulizike ni mapenzi ya Mungu! Kazi ya Mungu haina makosa! Marehemu atabaki daima kwenye kumbukumbu ya mioyo yetu! Pengo lake haliwezi kuzibika tena! Sisi tulimpenda, lakini Mungu alimpenda zaidi! Bwana alitoa, na Bwana ametwaa, jina la Bwana na libarikiwe! nk.

Wakati mwingine inawekwa kanda ya muziki wa nyimbo za maombolezo. Pengine zinachapishwa hata kadi za ukumbusho na kuvaliwa sare za msiba nk. Yote hii ni kwa ajili ya kutuliza wafiwa. Lakini hata hivyo unaona wafiwa hawatuliziki sana wanazidi kuwa na majonzi na kubujika machozi. Hiyo ndiyo hali halisi inayoletwa na kifo. Kumbe ingefaa zaidi katika mazingira kama hayo kukitafakari kifo. Na katika misiba ya kikristu yatakiwa kutafakari kuhusu mwanga huu anaotupatia Kristu, yaani tumaini la ufufuko.

Hebu sasa tumfuatilie Yesu anapofika msibani anakabilianaje na mazingira haya magumu ya uchungu na huzuni? Atawatulizaje wafiwa hawa? Aidha wafiwa wenyewe wanamtazamaje Yesu aliyechelewa kufika licha ya kuambiwa hali ya mgonjwa kabla hajafa? Vituko anavyovionesha Marta kwa Yesu vinawakilisha vituko na fikra za wengi wanapokabiliwa na msiba au matatizo mazito. Mara nyingi tunasikia hata watu wa dini wanapokuwa katika matatizo, wanakosa imani, wanamkasirikia Mungu, wanakatishwa tamaa ya kuamini.

Angalia sasa Yesu anapofika pale msibani Marta anaanza kumvaa na kumgombeza bila hata ya kumwamkia: “Bwana kama ungalikuwapo hapa ndugu yangu hangalikufa.” Yesu anamwelewa vizuri tu Marta anajaribu kumtuliza kwa maneno aliyozoea kuyasikia mfiwa kadiri ya fikra za wengi ili aweze baadaye kuyatolea maelezo ya kina anamwambia: “Usijali ndugu yako atafufuka.” Kwa jibu hilo la Yesu, Marta anazidi kuchafuka nyongo tu, kwani haoni jipya kwa sababu alishakeremishwa ukweli huo kwenye imani ya mafarisayo juu ya ufufuko ujao kwa hiyo mara moja anamdakiza Yesu: “Najua ya kuwa atafufuka katika ufufuo siku ya mwisho.” Ni dhahiri kwamba uelewa huu wa ufufuko ujao hauna maana yoyote.

Ufufuko utakaokuwepo sijui lini, yaani Mungu atuache tufe kisha baada ya kupita miaka mingi aturudishie tena maisha haya. Imani ya mtindo huu haiwezi kumtuliza mtu. Kutokana na udhaifu huo wa hoja ya ufufuko wa siku ya mwisho, Yesu anaongeza maneno yanayoleta maana na yanauyotuliza anamwambia kwa mkazo: “Mimi ndimi huo ufufuo na uzima.” Kumbe kama tuko gizani, basi tunahitaji mwanga toka nje unaoweza kutuangaza. Kujijulisha namna hii kwa Yesu kunafanana na kule alikomwambia yule Msamaritana pale kisimani: “Mimi ninayesema nawe, ndiye.”

Ni mimi niliye hapa ndiye ninayeweza kuhuisha mambo, ninayeweza kuwatuliza, wale waliokata tamaa ya maisha. Hapa mpangilio wa maneno unaanza na ufufuo halafu Uzima. “Mimi ndimi ufufuo na uzima”. Yaani kwanza kuwekwa huru halafu kuishi milele. Ufufuo ndiyo kitu cha muhimu zaidi katika maisha yetu ya sasa. Ufufuo ni mwito hasa kwa walio wazima kimwili halafu kwa waliokufa. Sisi tumeshakuwa wafufuka anavyosema Paulo: “Hata wakati ule tulipokuwa wafu kwa sababu ya makosa yetu, alituhuisha pamoja na Kristo; yaani, mmeokolewa kwa neema. Akatufufua pamoja naye, akatuketisha pamoja naye katika ulimwengu wa roho, katika Kristo Yesu.” (Efeso 2:5-6). Ni kwamba mtu huyu amepata maisha au uzima ambao hauwezi kumtoka kutokana na kufa kibaolojia.

Maisha ya mbinguni ni bora zaidi kuliko maisha ya duniani. Jaribu kupata picha ya watoto pacha walio bado tumboni mwa mama. Humo tumboni watoto hao wanalishwa chakula toka mwilini mwa mama yao. Inapotokea kwamba mmoja anatangulia kuzaliwa, yule aliyebaki tumboni anaweza kuwaza kwamba mwenzangu amekufa. Lakini yule aliyezaliwa na kuona mwanga anaufurahia uso wa mama yake ambao kabla yake hakuujua ulivyo ingawaje mama yake huyo ndiye aliyekuwa anampa uhai alipokuwa bado tumboni. Sasa anauona laivu uso wa mama yake. Vivyo hivyo Yesu anaposema anayenisadiki mimi hatakufa anamaanisha kwamba baada ya maisha haya kuna maisha mengine utakayoyaona laivu.

Dada mwingine, Maria naye anafika kwa mtindo wake. Yeye anafika huku analia. Yesu anapomwona Maria analia anamwelewa kwamba hayo ni mapato ya kifo ndiyo yanayofanya mtu alie. Lakini kilio cha Maria na cha waombolezaje wengine ni kile cha sauti na cha kukata tamaa. Tofauti na kilio cha Yesu baada ya kuuliza: “Mmemweka wapi?” Yesu analia, lakini kilio chake hakikuwa cha kukata tamaa bali yasemwa yalikuwa yanamtoka tu machozi. Kwa hiyo hata mtu mwenye imani yatamtoka tu machozi mbele ya kifo. Baada ya kuelewana hivyo juu ya ufufuo na uzima, sasa Yesu anaanza kufanya vitu vyake ambavyo ndiyo ishara inayoonesha kuwa yeye ni ufufuo na uzima. Hapa Kifo kinakatwa kilimilimi.

Yesu anaagiza kuliondoa jiwe lililofunika pango alimowekwa mfu. Kuliweka jiwe juu ya pango maana yake ni kuliziba. Kitendo hiki cha kufunika kinatafsiriwa kuwa ni cha kusahau. Kwamba kesi ya mtu aliyekufa imeisha. Hebu ifunike! “Funika kikombe mwanaharamu apite”. Kumbe Yesu anaagiza: “Liondoeni jiwe.” Kwa sababu haina maana kuufunika kwa jiwe ulimwengu wa wazima katika shimo la “sahau” na kumtenga na ulimwengu wa watu walio paradizini. Martha anapata bado shida ya kuelewa maana ya kutoa jiwe lile wakati mambo yameishaharibika kabisa na yananuka.

Bado ana mashaka, akdhani kwamba mambo yataweza kumzidi Yesu. Anadadisi: “Ananuka kwa vile amekaa humo siku nne.” Marta hajui kwamba kunuka ndiyo pia ni hali halisi ya kifo. Yesu anamwambia: “Marta kama unasaidiki, utaona utukufu wa Mungu.” Baada ya kufunguka macho yabidi kuangalia mambo kwa undani zaidi na kuona mambo ambayo macho ya kawaida hayawezi kuyaona. Maana yake, kama unasadiki utaweza kuona.

Toka hapa sasa kunafuata mahitimisho ambayo ndiyo uhondo wa Injili yote ya leo. Yesu analia kwa sauti kuu: “Lazaro njoo huku nje.” Hiyo sauti ni kilio cha ushindi. “Mfu akatoka,” huyo anatamkwa jina la mfu na siyo kwa jina la Lazaro. Mfu alitoka aliyeviringishwa sanda miguuni, mikononi na uso umefungwa leso. Mfu huyo hatuoni wala sisi hatumwoni. Ameviringishwa nguo na kufunikwa leso kama vile mtoto mchanga aliyezaliwa.

Hapa ni dhahiri kwamba tunaletewa fundisho muhimu sana la kiteolojia, kwamba hata Lazaro amezaliwa toka tumbo la kaburi. Ni ukweli usiopingika kwamba Yesu amemhuisha Lazaro. Mwinjili anataka kurudia tena ishara ambayo Yesu ameitoa katika kitendo hiki cha kumfufua Yesu kuwa ni Bwana wa maisha, Bwana wa uzima siyo uzima huu wa kibaolojia wa kurudishia uhai Lazaro, la hasha, bali mwuujiza huo tuuchukulie kuwa ni ishara au kichokoo tu cha kutuonesha au kutushirikisha uzima mwingine ambao Yesu amekuja kutuletea hapa ulimwenguni. Mfu anakuwa mzima anazaliwa upya na anabaki katika hali ya mfu ameviringishwa vitambaa. Yaani mfu ambaye Yesu anamwita toka kaburini (pangoni) anabaki bado na alama zote za mzikwa wa kaburini. Kisha Yesu anasema: “Mfungueni, mkamwache aende zake.” Usemi huu nao ni muhimu sana. Tamko hili ni fumbo, kwani Yesu hasemi, “twendeni naye pamoja anakoenda huko”.

Baada ya tamko hili la Yesu na kumfungua mfu na kumwacha aende zake, tungetegemea kuona vituko vingine husika vikiendelea kuorodheshwa. Yaani tungemtegemea Yesu anaendelea kutoa maagizo yafuatayo: “Mfungueni halafu akisha jiweka sawa, ataweza kuja kutusimulia mambo yalivyokuwa kuzimuni alikokuweko siku hizi nne. Kisha tutaenda kumnywea na kufanya sherehe. Ratiba nyingine itaendelea jinsi mambo yatakavyojitokeza.”

Pengine hata Lazaro mwenyewe angeenda kumkumbatia Yesu ikiwa kama ishara ya shukrani. Lakini kumbe Yesu anasema tu “mfungueni na mkamwache aende zake.” Lazaro anaondoka na kwenda zake kimyakimya bila ya kuwahamasisha, au kuwachangamsha waliokuwa wanahuzunika.

Ndiyo mwisho! Ndivyo anavyotutendea Mungu, anayetuumba, anatuacha mahuru tuendelee na maisha bila kutufunga. Hii ni ishara kubwa katika maisha yetu ya kidini, kutomfunga Mungu katika imani, bali kumwacha huru. Ishara hiyo pia ni mwito kwa ndugu wanaolia na kuhuzunika kwa kuondokewa na ndugu, rafiki na mpenzi wao, lakini utakuwa ni ubinafsi mkubwa sana kumshikilia na kumtaka marehemu aendelee kubaki nao.

Yabidi kumwacha “kumfungua na kumwacha aende kwa raha zake.” Ingependeza sana kutanguzana naye kwenda pamoja huko aendako. Kumbe haiwezekani! Sisi tubaki tu kumsindikiza kwa jicho la imani katika hatua mbalimbali za maisha yake. Tumwache aende kwa uhuru wake wote. Ama kweli mwisho wa maisha ni mwanzo wa maisha.

Padre Alcuin Nyirenda, OSB








All the contents on this site are copyrighted ©.