2014-04-05 09:00:28

Kanisa ni Mama na Mwalimu!


Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican inapenda kukushirikisha na kukumegea mchango uliotolewa na Wenyeheri Yohane XXIII pamoja na Yohane Paulo II katika maisha na utume wa Kanisa mintarafu Mafundisho Jamii ya Kanisa. Leo katika makala haya tunazama zaidi katika kupembua mchango wa Mwenyeheri Yohane XXIII. RealAudioMP3

Maana ya mafundisho jamii ya Kanisa: Ni mkusanyiko wa mawazo na mafundisho kuhusu jamii, ambayo Kanisa limekuwa likiyatilia mkazo, hasa kuhusiana na maswala ya haki jamii, umaskini, utajiri, maswala ya uchumi, muundo wa jamii na wajibu wa Serikali za nchi katika kukabiliana na maswala hayo kwenye jamii husika.

Mafundisho haya yanapata chimbuko lake katika Waraka wa kwanza kabisa kuhusu maswala ya jamii, ulioandikwa mnamo mwaka 1891 na Papa Leo XIII, ambao unajulikana kwa jina la Rerum Novarum, “Mambo Mpya” Lakini kwanza kabisa, Mafundisho Jamii ya Kanisa yanapata chumbuko lake katika Maandiko Matakatifu, Maandishi na mawazo ya Mtakatifu Thomas wa Aquino na mafundisho ya Mtakatifu Augustino, Askofu na Mwalimu wa Kanisa kuhusu maswala ya jamii. Mafundisho jamii ya Kanisa yamesimikwa kwenye nguzo kuu tano:

Manufaa ya wote, Mshikamano, kusaidiana kwa kujikita katika kanuni ya auni, upendeleo wa pekee kwa maskini zaidi katika jamii, mali yote iliyopo duniani ni kwa ajili ya matumizi ya wanadamu wote. Nguzo hizi tano zinapata chimbuko lake katika: Maandiko Matakatifu, Mapokeo ya mababa wa Kanisa na Nyaraka mbalimbali zinazotolewa na Khalifa wa Mtakatifu Petro pamoja na zile zinazotolewa na viongozi wa Makanisa mahalia popote duniani.

Kwa hayo maelezo mafupi, tunaweza sasa kuona ni jinsi gani hawa mapapa wawili ambao mama Kanisa atawatangaza watakatifu, walichangia kwa njia ya mafundisho yao katika kuendeleza Mafundisho Jamii ya Kanisa. Katika makala haya tutaanza kwa kuchambua mchango uliotolewa na Papa Yohane XXIII katika mchakato wa maisha na utume wa Kanisa mintarafu Mafundisho Jamii.

Papa Yohane XXIII : Kanisa ni Mama na Mwalimu; Amani Duniani
Angelo Giuseppe Roncalli alizaliwa kwenye familia maskini ya wakulima huko Bergamo- kaskazini mwa Italia mnamo tarehe 25 Novemba 1881, akiwa ni mtoto wa nne kati ya watoto kumi na watatu. Familia yake iliishi maisha bora ya Kikristo na ilijishughulisha sana na maswala ya kanisa. Mjomba wake mmoja Zaverio, alichangia sana katika makuzi ya kiroho na ya kiutu ya Angelo Giuseppe Roncalli. Mjomba huyu alikuwa ni mwanaharakati wa chama cha “Catholic Social Action” ambacho kilikuwa kimeanzishwa wakati ule na Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Bergamo ili kusaidia maswala ya jamii.

Hili ni jambo ambalo lilikuwa limehimizwa sana na Papa Leo wa XIII kwenye waraka wake wa jamii Rerum Novarum au kwa lugha ya kiswahili Mambo mapya, akimaanisha mabadiliko yaliyokuwa yanatokea kwenye Bara la Ulaya wakati wa Mapinduzi ya Viwanda na jinsi ambavyo miundombinu hii, pamoja na kwamba, ilikuwa ni hatua kubwa ya maendeleo, lakini iliwaathiri wafanyakazi ambao walijikuta wakipunguzwa au kuachishwa kazi kutokana na kwamba kazi walizokuwa wakizifanya kwa mikono, sasa kwa asilimia kubwa zilikuwa zinafanyika kwa mashine na hivyo uwepo wao katika viwanda haukuonekana tena kuhitajika.

Jambo hili lilisababisha umaskini mkubwa wa hali na kipato katika jamii licha ya mabadiliko yaliyotokea katika sekta ya uchumi na maendeleo. Mambo haya yalikuwa yanatokea hata nchini Italia, na ndiyo maana, jimbo la Bergamo lilikuwa linajitahidi kuganga machungu ya watu waliokuwa wanaendelea kuathirika kutokana na mabadiliko hayo.

Baada ya kupewa Daraja la Upadre, Padre Angelo Roncalli alifanya utume waka katika hospitali kama mhudumu wa kiroho. Vile vile, wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia alikuwa akitoa huduma za kiroho kwenye kambi za kijeshi. Yale aliyoyaona kutokana na matukio yale yalimfanya aamini kwamba “ kwa kweli vita ni shetani mkubwa”. Kazi zake za kitume zilimlazimu kutoka nje ya Italia.

Historia ya maisha yake inaonesha kwamba, kuanzia mwaka 1924 hadi 1934 Padre Angelo Roncalli alikuwa mwakilishi wa baba mtakatifu katika nchi ya Bulgaria. Na kuanzia mwaka 1934 – 1944 alikuwa mwakilishi wa Papa katika nchi ya Uturuki na Ugiriki. Katika nafasi hizi za kitume, aliweza kukuza muono wa kiekumene na ule wa majadiliano na watu wa imani mbalimbali. Mwisho mwa mwaka 1944 padre Angelo Roncalli aliteuliwa kuwa Balozi wa Vatican nchini Ufaransa. Akiwa katika wadhifa huo huko Ufaransa, alikuwa pia Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa. Akiwa katika utume huu alijifunza kwamba, inawezekana kabisa kuweka pembeni tofauti za misimamo ya kisiasa ambazo na kufanya “mazungumzo na watu wote wenye mapenzi mema”.

Katika uhusiano wake na wale ambao hawakuwa na imani Katoliki, alijaribu kuangalia zaidi mambo yale yanayouwanganisha na Wakatoliki, zaidi kuliko kuangalia yale yanayowatenganisha. Hii ikawa ni chemchemi ya majadiliano ya kiekumene na kidini; mambo yaliyovaliwa njuga na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican na bado yanaendelea kupewa kipaumbele cha pekee na Kanisa Katoliki katika maisha na utume wake, ili dunia iweze kuwa ni mahali pazuri pa kuishi watu wakiheshimiana na kuthaminiana kama ndugu, licha ya tofauti zao za kiimani, kisiasa na kitamaduni.

Mnamo mwaka 1953 aliteuliwa kuwa askofu mkuu na patriaki wa Venice- Italia. Angelo Roncalli alichaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki kama Khalifa wa Mtakatifu Petro mnamo tarehe 28 Oktoba 1958, mwezi mmoja kabla ya kutimiza umri wa miaka sabini (70). Alichagua jina Yohane wa XXIII, na aliliongoza Kanisa kwa kipindi cha miaka minne na miezi saba.


Dunia ikiwa katika hali ya vita baridi, mwaka 1959 Papa Yohane XXIII aliutangazia ulimwendu nia yake ya kuitisha Mtaguso Mkuu ili kuleta upyaisho (aggiornamento) katika Kanisa; na kubadili mtazamo wa Kanisa kuelekea jamii, ili Kanisa liwe wakala wa umoja na haki. Kadiri mipango ya kufanya mtaguso ilivyozidi kusonga mbele, ilikuwa wazi kwamba papa angeelekeza nguvu zake kwanza kabisa kwenye maswala ya ndani ya Kanisa, yaani: Liturujia, Utume wa Askofu mahalia, asili ya Kanisa na kadhalika.

Kwa hiyo, tunaweza kusema kwamba, Baba Mtakatifu alikuwa na ajenda tatu katika utume wake kama khalifa wa mtakatifu Petro. Ajenda ya kwanza ilikuwa ni upyaisho wa Kanisa, (kuleta mabadiliko ndani ya Kanisa) “aggiornamento” jambo la pili lilikuwa ni Umoja wa Madhehebu ya Kikristo; na jambo la tatu ni umoja na amani kati ya watu wa mataifa au amani duniani. Mtaguso wa Kiekumene ndio ulipaswa kuleta haya mabadiliko ndani ya Kanisa Katoliki, na baada ya hapo kutoka kifua mbele kwa ajili ya kuanza majadiliano na makanisa mengine ya kikristo na kuingia kwenye umoja wa kiekumene.

Hali ilivyokuwa duniani wakati wa uongozi wa Papa Yohane XXIII kama Khalifa wa Mtakatifu Petro
Katika kipindi cha uongozi wa papa Yohane wa XXIII jumuiya ya kimataifa ilikuwa inapita kwenye mabadiliko mengi kijamii, kisiasa na kiuchumi. Itakumbukwa kwamba ni kwenye mwaka 1959 Rais Fidel Castro na jeshi lake wanachukua madaraka huko Cuba na Havanna kwa ujumla; mwaka huo huo John Kennedy anachaguliwa kuwa Rais wa Marekani; mwaka 1960 unaundwa Umoja wa nchi zinazo uza na kusambaza petroli nje ya nchi zao (OPEC); mwaka huo huo Marekani inaingia kwenye mgogoro wa kivita na nchi ya Vietnam; Ukuta wa Berlin unajengwa; mwanadamu wa kwanza anafanya safari kwenye sayari kuizunguka dunia mnamo mwaka 1961; makombora ya Urusi nchini Cuba yanasababisha mgogoro kati ya Marekani na Umoja wa Kisovieti, mgogoro ambao ulikuwa karibu unafikia ukingoni mwa kuanza vita vya nyuklia. Ni mwaka ambao pia nchi nyingi za Afrika, moja baada ya nyingine, zinaanza kujipatia uhuru wa bendera kutoka kwa wakoloni.

Katika matukio haya yote, Papa Yohane XXIII alitaka Kanisa litoe mchango wake katika kukabiliana na hali hii iliyokuwa inaukumba dunia. Ila kwa namna moja au nyingine, Kanisa hadi kipindi kile halikuwa na mtizamo wa kijamii na wala mchango wake haukuwa unajulikana wala kuonekana katika matukio yote hayo. Hivyo basi, jambo la kwanza alilofanya Papa Yohane XXIII ni kulitambulisha Kanisa kwa dunia nzima.

Baba Mtakatifu Yohane XXIII alilitambulisha Kanisa kama "Mater et Magistra", yaani Kanisa ni Mama na Mwalimu wa mwanadamu. Kwa kulitambulisha Kanisa kwa namna hii, Papa Yohane wa XXIII alikuwa na lengo la kulifanya Kanisa libadili mwelekeoo lililokuwa nao hadi kipindi kile na alitaka kulitumikia kama wakala wa Umoja wa Wakristo na kuisaidia jamii ili iweze kushughulikia maswala ya ukosefu wa haki kwenye maswala ya uchumi, tishio la vita ya nyuklia na migogoro kati ya mataifa. MM ilitolewa rasmi mnamo mwezi Julai 1961 mwaka mmoja na miezi mitatu kabla ya kuanza kwa mtaguso, na PT ilitolewa wakati Mtaguso ukiendelea, yaani tarehe 11 Aprili 1963. MM ilileta mtazamo mpya kwenye tafakari ya Kanisa juu ya masuala ya kijamii. Waraka huu ulitolewa kwanza kabisa kwa ajili ya kuadhimisha miaka 70 ya RN.

Usikose kumshirikisha jirani yako mchango uliofanywa na Mwenyeheri Yohane XXIII katika maisha na utume wake mintarafu Mafundisho Jamii ya Kanisa. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican itaendelea kukujuza kwa kina na mapana mchango wa Wenyeheri Yohane XXIII na Yohane Paulo II, wakati huu Mama Kanisa anapoendelea kujiandaa kuwatangaza kuwa ni Watakatifu, hapo tarehe 27 Mei 2014, Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro pamoja na viunga vyake, vitakapowaka kwa moto wa furaha!








All the contents on this site are copyrighted ©.