Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya Tano ya Kipindi cha Kwaresima
Mpendwa msikilizaji wa Radio Vatican, tunaendelea na tafakari masomo Dominika ya V
ya Kipindi cha Kwaresima. Neno la Mungu latualika kutambua kuwa Kristu ndiye mfalme
na chanzo cha maisha yetu.
Katika somo
la kwanza toka katika kitabu cha Nabii Ezekieli tunakutana na Mungu ambaye anapeleka
ujumbe wake kwetu kwa njia ya Ezekieli akisema nitawaondoeni kutoka makaburi yenu
na kuwapandisha kwenda nchi ya Israeli. Ezekieli anakuja na habari hii wakati Waisraeli
pamoja naye wakiwa utumwani Babeli katika karne ya 6 hivi. Kumbuka Ezekieli alikuwa
kasisi aliyepelekwa uhamishoni mnamo mwaka 587KK.
Huko Babeli watu walipata
taabu na kukata tamaa na hivi wakawa kama kondoo asiye na mchungaji. Ni kwa sababu
hiyo basi Mungu anamtuma Ezekieli kuwatangazia uhuru na kamilisho la ahadi zake, yaani
atawarudisha katika maisha mapya, atawatoa katika makaburi yaani toka utumwani na
kuwarudisha katika nchi yao.
Ujumbe huu unagusa maisha yetu hivi leo, pale
ambapo tunazama katika dhambi na kuacha maisha ya kutimiza mapenzi ya Mungu, tunaingia
makaburini. Zaidi ya hilo, vita, madhulumu mbalimbali, uvivu, madawa ya kulevya na
magomvi pengine katika familia au katika sehemu zetu za kazi ni alama hakika za utumwa
na angamizo la uhuru wetu na hivi kifo. Leo Mungu anatuambia nirudieni mimi nami nitawatoa
katika makaburi yenu hayo na kuwarudishia uhai.
Mtakatifu Paulo akiwaandikia
Warumi, anawakumbusha wajibu wa kuwa na roho wa Mungu ndani mwao kama kigezo cha kumpendeza
Mungu. Ndiyo kusema wale wafuatao matendo ya mwili wako nje ya mstari wa kutimiza
mapenzi ya Mungu. Akikazia fundisho hili anasema Kristu aliweza kufufuka kwa sababu
alikuwa na roho wa Mungu katika ukamilifu wake.
Ni kwa jinsi hiyo mambo ya
kidunia yaani ya kimwili hufa na yatapita lakini yaliyo ya kiroho yaani yaongozwayo
na Kristo mwenyewe hayatapita kamwe, bali kuingia katika utukufu wa Mungu kama Kristu
mwenyewe alivyoingia. Katika ubatizo tulipokea roho wa Mungu na hivi hata kama maisha
yetu yatapita katika ulimwengu huu, lakini haitakuwa mwisho wa kila kitu bali yatageuzwa
na kuwa maisha mapya.
Katika somo la Injili mada ni ileile ya yakuwa Bwana
ndiye chanzo cha maisha yetu na ndiye atupaye uhai. Bwana atamfufua Lazaro na kumrudishia
uhai akithibitisha ukuu wa Mungu na kutaka kujenga imani ya wafuasi wake. Yapo mambo
kadhaa ya kuangalia kwa makini katika Injili hii. Jambo la kwanza tunakutana na watu
watatu yaani Martha, Mariamu na Lazaro yaani kaka na dada wawili. Hawa ndugu haioneshwi
wazazi wao wala ndugu wengine wa karibu, ndiyo kusema tunagundua mwandishi ataka kutuambia
juu ya JUMUIYA YA KIKRISTO ambamo hakuna mabwana na watwana, bali wote ni kaka na
dada, yaani NDUGU!
Mpendwa msikilizaji, Bwana anapopata taarifa kwamba Lazaro
anaumwa haendi huko mpaka atakapofariki na tena baada ya siku nne, Je, alitaka afe?
Kwa nini Bwana analia wakati anajua atamwondoa katika mauti Lazaro? Kwa nini Bwana
haingia Bethania mara moja? Mpendwa msikilizaji kumwacha Lazaro afe anataka kutufundisha
kuwa hakuja kuzuia kifo cha mwili, hakuja kuzuia mtiririko asili wa mambo yamhusuyo
mwanadamu, ndiyo kusema hakuja kufanya maisha ya hapa duniani yawe ya milele bali
kuyageuza na kuwa maisha mapya yatakayokuwa ya milele.
Kumbe mpendwa msikilizaji,
mwili ni lazima utakufa kama njia ya kuingia maisha mapya. Katika hili yafaa kutafakari
vema majadiliano kati ya Bwana na Martha ambayo hitimisho lake ni katika maneno ya
Bwana akisema âaniaminiye mimi hatakufa kamwe. Bwana anaenda kwa ndugu hawa baada
ya siku nne, kwa sababu katika utamaduni wao ilisadikika kwamba katika siku tatu mtu
alikuwa hajafa kikamilifu, kumbe ukamilifu wa kifo na ondoko la maisha lilikuwa baada
ya siku nne. Lengo la mwinjili ni kutaka kutuambia si jambo jingine bali yakuwa Lazaro
alikuwa amepoteza uhai kabisa.
Bwana anapofika katika kaburi la Lazaro analia,
na hili linatushangaza kwa sababu alitambua kuwa baada ya muda mfupi atarudisha uhai
wake! Katika hali ya kawaida jamaa yetu anapokufa tunalia. Tunalia si kwa sababu ndugu
huyu hatafufuka bali kwa sababu kwa kitambo kifupi hatutamwona. Ni alama na ishara
ya upendo kwa ndugu zetu. Hata hivyo yafaa kutambua kuwa kuna kilio kilichojaa matumaini
kama kilio cha Bwana kwa Lazaro na kilio kisichojaa matumaini, ambacho huona kifo
kama mwisho wa kila kitu. Sisi wakristo na watu wenye mapenzi mema yatupasa kulia
kama Bwana, tukikazia mapenzi ya Mungu yafanyike na hivi kukazia sala zaidi kwa ajili
ya aliyeaga dunia!
Mpendwa msikilizaji, Bwana ataomba liondolewe jiwe juu
ya kaburi la Lazaro. Katika utamaduni ule, jiwe lilimaanisha kutenganisha maisha na
kifo, dunia ya waliokufa na waliohai, sasa Bwana anataka wakristu waachane na mantiki
hii na waishi mantiki ya ufufuko wa Bwana yaani hakuna tena utengano kati yetu na
Mungu.
Tukimalizia kujibu swali lisemalo kwa nini Bwana haingia Bethania mara
moja, tunaitwa kutambua kuwa Bwana hawezi kuingia katika nyoyo zetu kama zimekata
tamaa. Kumbuka, Bethania wanalia kwa sababu ya kifo cha Lazaro na hivi lazima watoke
kwanza katika shida hiyo, wajenge tumaini katika Bwana na kisha ataingia katika kijiji
chao. Bwana ni maisha, ni tumaini, ni furaha na alipo yeye hakuna kifo, hakuna kilio
bali tumaini katika ufufuko.
Mpendwa ninakutakia furaha na matumaini katika
maisha yako daima ukimtanguliza Mungu na kwa nguvu zake kukua na kusimamia matumaini
na ukuu wa Kristu anayetupatia maisha akituondoa kutoka katika upotofu wa dhambi na
kutuingiz katika mwanga wa imani zawadi maisha na uzima wa milele. Tumsifu Yesu Kristo.
Tafakari hii imeletwa kwako na Pd Richard Tiganya C.PP.S.